Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge kuijadili miswada ya sheria za uchaguzi siku nne

Bunge Pic Data Wabunge kuijadili miswada ya sheria za uchaguzi siku nne

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miswada mitatu ya sheria za uchaguzi kuanza kujadiliwa bungeni kwenye mkutano wa 14 wa Bunge la 12, unaoanza kesho Jumanne, Januari 30, 3034.

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa kimataifa iliyotolewa jana, mkutano huo umeongezewa wiki moja na hivyo kufanyika kwa wiki tatu badala ya mbili kama ilivyozoeleka.

Taarifa hiyo ilisema mkutano huo umepangwa kufanyika kuanzia kesho Jumanne hadi Februari 16, 2024, jijini Dodoma.

Imesema hilo limefanyika kutokana uzito wa majukumu yaliyopangwa ikiwemo uzito wa miswada itakayoshughulikiwa.

Miswada iliyopangwa kujadiliwa katika mkutano huo ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023.

Miswada mingine ni Muswada wa Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 na Muswada wa marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2023.

Aidha, taarifa hiyo imesema katika mkutano huo kamati za kudumu za Bunge zitawasilisha taarifa za shughuli zilizotekelezwa na kamati kwa mwaka 2023.

Pia, wastani wa maswali 250 ya kawaida na maswali 24 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa na wabunge.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge, miswada hiyo itaanza kujadiliwa leo Jumanne na kuhitimishwa Februari 2, 2024.

Miswada hiyo ilisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba 10, 2023 na kupelekwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa ajili ya kujadiliwa na kuchambuliwa.

Kamati hiyo ilipokea na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali kwa muda wa siku nne mfululizo kuanzia Januari 6 hadi 10 mwaka 2024, ambapo ilipokea maoni kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali 1,707.

Baadhi ya maoni yaliyowasilishwa kwenye kamati hiyo ni kutaka wakurugenzi wa halmashauri kutosimamia uchaguzi, kuwepo kwa kifungu kinachotoa kigezo cha ushindi wa kura za urais ziwe zaidi ya asilimia 50, vyama vya siasa vyote kupewa ruzuku na uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na si Tamisemi.

Maoni mengine ni kuondolewa kwa gharama za kuchukua fomu, vyama kulazimishwa kuteua asilimia 50 ya wagombea wanawake katika chaguzi ili kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi na kurekebishwa kwa kifungu kinachoeleza uteketezaji wa nyaraka za uchaguzi baada ya miezi sita.

Hata hivyo, Chadema ambacho ni miongoni mwa vyama 13 vya siasa vilivyowasilisha maoni yao kwenye kamati hiyo, kilipendekeza kufutwa na kuondolewa bungeni kwa miswada ya sheria hizo na badala yake muswada wa marekabisho ya Katiba upelekwe bungeni.

Januari 13, 2024, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alitangaza kufanyika kwa maandamano Januari 24 mwaka huu yaliyolenga kushinikiza kuondolewa bungeni kwa miswada hiyo mitatu ya uchaguzi pamoja na ugumu wa maisha.

Maandamano hayo yaliyoruhusiwa na Jeshi la Polisi, yalifanyika jijini Dar es Salaam Januari 24, mwaka huu kuanzia Mbezi Mwisho na Buguruni kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) zilizopo barabara ya Sam Nujoma, Ubungo walipokabidhi ujumbe wao ili kupelekwa makao makuu ya UN, New York nchini Marekeani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live