Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge Mollel, Musukuma na mkurugenzi wa halmashauri wapamba mkutano wake

10256 DC+PIC TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mkuu mpya wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya ameahidi kula sahani moja na baadhi ya wanasiasa wilayani humo wanaomkashifu Rais John Magufuli kupitia kwenye nyumba za ibada na mikutano ya hadhara.

Alitoa kauli hiyo juzi katika uwanja wa Shule ya Msingi Sambasha katika mkutano aliouitisha kuwaaga wananchi wa kata hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Sabaya ni diwani wa Sambasha pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Arusha.

Katika mkutano huo, Sabaya aliambatana na mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma; mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel na baadhi ya madiwani wa chama tawala jimbo la Arumeru Magharibi.

Sabaya alisema wakati Rais Magufuli anahangaika kujenga viwanda pamoja na shida za watu wanyonge, baadhi ya wanasiasa wanakesha wakimtukana hata kwenye nyumba za ibada wilayani Hai.

Bila kuweka hadharani majina ya wanasiasa hao, Sabaya alisema anawatumia salamu na anaamini kuanzia sasa hawatarudia kumtukana Rais Magufuli ovyo. Hai mbunge wake ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Rais anahangaika na viwanda, anahangaika na shida za wanyonge nadhani hawatarudi tena kuzungumza maneno hayo ya kumtukana Rais Magufuli tena kanisani,” alisema Sabaya.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Musukuma alisema ndani ya CCM mtu akifanya jambo la maana ataandamwa na kumtaka Sabaya kushughulika na maisha ya wanyonge na kutojali vikwazo atakavyokumbana navyo.

Hatua ya Musukuma kuhutubia mkutano kwa mwaliko nje ya jimbo lake, inaonekana kufanana na ya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliyehutubia mkutano wa hadhara Jimbo la Kilwa Kusini mkoani Lindi kwa mwaliko wa mbunge Suleiman Bungara maarufu Bwege.

Hata hivyo,Agosti mosi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alimpa siku mbili Zitto kujisalimisha kwa kamanda wa polisi mkoani Lindi kwa tuhuma za kufanya mikutano nje ya jimbo lake na kutoa kauli za uchochezi. Agizo hilo halijatekelezwa.

Ang’atwa sikio

Naye diwani wa Musa, Flora Zelothe alimweleza Sabaya kuwa anapaswa kuhakikisha anatimiza ndoto ya ujenzi wa wodi ya wanawake katika zahanati ya kata hiyo kwa kuwa ni ahadi aliyoitoa wakati wa uchaguzi 2015.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Dk Wilson Mahera aliwaambia wakazi wa kata hiyo kwamba licha ya diwani wao ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, waondoe hofu kwa kuwa Serikali itendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz