Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge EALA wapanda miti UDOM

Sun, 22 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) watatakiwa kupanda miti wanapoanza masomo, watapimwa wanavyoitunza na kupewa maksi za utunzaji wake wakati wanapohitimu masomo chuoni hapo.

Mwenyekiti wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Dk Abudullah Husnuu Makame amewapa changamoto hiyo wahadhiri na wanafunzi wa Udom baada ya wabunge hao kushiriki katika kampeni ya kupanda miti ya mikorosho chuoni hapo.

Dk Makame alisema chuo kinatakiwa kuweka mkakati wa kupanda miti takribani milioni kwa mwaka na hiyo itafikiwa kama kila mwanafunzi anapanda miti mitatu au zaidi, anaitunza na anapohitimu anapewa maksi kutokana na kutunza miti yake.

"Kampeni hiyo ya kila mwanafunzi kupanda miti itasaidia kuifanya Udom ya kijani kwani kutakuwa na miti ya kutosha na wanafunzi wataitunza kwani wanajua mwisho wa masomo watapewa maksi za kuchangia kufaulu masomo yao," amesema Dk Makame.

Mbunge wa EALA kutoka Uganda, Mathias Kassamba alisema kampeni ya kukifanya chuo cha Udom cha kijani, itafanikiwa tu kama chuo hicho kitaanzisha vitalu vya miche ya kutosha ya miti ili kufanikisha upandaji wa miti chuoni hapo.

Kassamba alisema kuwepo kwa vitalu vya miche chuoni kutahamasisha wanafunzi zaidi ya 25,000 kupanda miti katika mazingira hayo na kutengeneza vivuli, matunda na chakula kwa ajili yao na vizazi vijavyo na kuongeza vitalu hivyo vitakuwa chachu ya kufanikisha kampeni ambao itawafanya wanafunzi wote na watumishi kupanda miti kutokana na kuwepo kwa miche ya kutosha chuoni hapo.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga alisema Udom kama imedhamiria kuweka azma ya kuwa kijani lazima ijikite katika kusaidia wananchi wanaoizunguka na wao wawe wa kijani.

Chanzo: habarileo.co.tz