Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge CCM wamwaga msaada Kisarawe

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe. Wabunge wa viti maalum CCM, Subira Mgalu na Zainab Vullu wametoa msaada wa  magodoro 20 na matangi mawili ya maji kwa ajili ya shule ya sekondari Maneromango.

Wametoa vifaa hivyo leo Ijumaa Januari 4, 2019 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa mbele ya Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara wilayani Kisarawe mwaka 2018.

Mgalu ambaye pia ni naibu Waziri wa Nishati amesema lengo la msaada huo ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo.

“Tunataka watoto wetu wafanye vizuri. Tulielezwa kuna changamoto ya magodoro na matangi  ya kuhifadhia maji tumewaletea. Hii yote ni kuondoa vikwazo vinavyoweza kusababisha wasiwe katika mazingira mazuri,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake Vullu amesema licha ya kuwa wilaya hiyo ina viwanda vingi lakini haviwezi kuwa na manufaa kama hakutakuwa na watu wenye elimu bora.

“Viwanda vinahitaji wafanyakazi na kama hatutasomesha watoto wetu basi ajira hizo zitakwenda kwa watu wa nje ya Kisarawe ni muhimu kwetu kuweka nguvu katika elimu,” amesema.

Akipokea msaada huo mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,  Jokate Mwegelo amesema vifaa hivyo vitaongeza kasi katika kutokomeza ziro.

Amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo wadau mbalimbali wameshiriki kuchangia fedha na vifaa mbalimbali na hadi sasa wamefanikiwa kujenga madarasa 10.

“Inaweza kuwa ndio kampeni ambayo imepata mafanikio makubwa zaidi kwa muda mfupi, ila sisi kwetu tunaona bado tunataka kuhakikisha mazingira ya elimu wilayani kwetu yanakuwa bora na watoto wanamaliza shule kwa ufaulu,” amesema Jokate.



Chanzo: mwananchi.co.tz