Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge CCM waja na staili mpya Mawenzi

10205 CCM+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wabunge wawili wa CCM jana walitumia mafanikio ya Diwani wa Kata ya Bomambuzi (CCM), Juma Raibu kumnadi mgombea wao wa udiwani wa kata ya Mawenzi mjini Moshi, Apaikunda Naburi.

Wabunge hao, Ester Mmasi wa viti maalumu na Dk Ngwaru Maghembe wa Bunge la Afrika Mashariki walisema uchapakazi aliouonyesha Raibu ndani ya miezi sita ndio atakaouonyesha Apaikunda.

Akimnadi mgombea huyo katika eneo la Aslam gereji, Mmasi alisema ndani ya miezi sita tangu achaguliwe kuwa diwani, Raibu amefanya mambo ambayo hayajawahi kufanywa na watangulizi wake.

“Ndani ya miezi sita amejenga madarasa Shule ya Msingi Mandela, amekarabati barabara za vumbi, amejenga kilometa tano za barabara ya lami, ametoa kadi 180 za bima ya Afya kwa wazee,” alisema.

Mbunge huyo pia alidai katika muda huo, ameanzisha kliniki kwa wagonjwa wa kisukari ambao hutibiwa bure na amefanikisha upatikanaji wa Sh400 milioni kwa ajili ya kituo cha Afya Pasua.

Kwa upande wake, Dk Maghembe alisema Raibu ameonyesha uchapakazi uliotukuka ndani ya miezi sita ikiwamo vita dhidi ya rushwa na uonevu na kusema Apaikunda naye moto ni huo huo.

Katika hatua nyingine, Meya wa Manispaa ya Moshi (Chadema) , Raymond Mboya amesema Sh400 milioni zilizopelekwa katika kituo cha Afya cha Pasua, ni mipango ya Baraza la Madiwani la Manispaa.

Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara jana kandokando ya barabara karibu na ofisi za CCM wilaya, kumnadi mgombea wa Chadema, Africana Mlay, Mboya alisema CCM wanapotosha kuhusu fedha hizo.

Kwa mujibu wa Mboya, kila mwaka Baraza la Madiwani linaoongozwa na Chadema hupanga mipango ya maendeleo, na safari hili lilipanga kiasi hicho cha fedha kipelekwe katika kituo hicho cha Afya.

Chanzo: mwananchi.co.tz