Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge 8 Dodoma, Pwani wanyimwa kura

148e5458d73407262aba94779ec3f20e.jpeg Wabunge 8 Dodoma, Pwani wanyimwa kura

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MCHAKATO wa kura za maoni kupata wagombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu ulimalizika jana na sasa walioongoza wanasubiri uamuzi wa vikao vya juu vya chama hicho vifanye uamuzi.

Kwenye Mkoa wa Dodoma wabunge watano waliomaliza mda wao wameanguka kwenye kura za maoni. Wabunge hao ni Omary Baduel Jimbo la Bahi, George Lubeleje wa Mpwapwa, Edwin Sanda, Kondoa Mjini, Joel Mwaka wa Chilonwa na Juma Nkamia, Chemba.

Wabunge waliomaliza muda wao na wameongoza kura za maoni ni Job Ndugai jimbo la Kongwa, Antony Mavunde Dodoma Mjini, Ashatu Kijaji wa Kondoa Vijijini, Livingstone Lusinde, Mtera na George Simbachawene, Kibakwe Baduel ameshindwa kwa kupata kura 32. Kenesi Nolo aliongoza kura 259, na Donald Mejitii kura 210. Kulikuwa na wagombea 36.

Katika Jimbo la Kondoa Mjini Ally Makoa aliongoza kwa kupata kura 137, akifuatiwa na Adam Kimbisa kura 71 na Sanda amepata kura 24. Kulikuwa na wagombea 47. Katika Jimbo la Mpwapwa, kulikuwa na wagombea 64, Lubeleje amepata kura 10 kati ya kura 659 zilizopigwa.

George Malima aliongoza kwa kupata kura 263, Charles Kuziganika kura 90, Zakayo Mkemwa kura 46, Charles Magaya kura 37, Juni Fusi kura 34, Islael Mhayo kura 15, Zakaria Magoye kura 13, na Njamasi Chiwanga kura 12.

Kwenye jimbo la Kibakwe kulikuwa na wagombea 19, Simbachawene aliongoza kwa kupata kura 667, Dk Kwame Mwaga kura 51, Agustine Galawika kura 19 na Frank Lubeleje kura 9. Katika jimbo la Kondoa Vijijini kulikuwa na wagombea 15, Dk Kijaji aliongoza kwa kupata kura 703, Hassan Lubuva kura 238, Issa Orry kura 36. Jimbo la Chemba lilikuwa na wagombea 20, Nkamia alipata kura 132.

Mohamed Moni aliongoza kwa kupata kura 327, Hawa Gondawe kura 66. Kwenye jimbo la Mtera Lusinde alipata kura 571, Dk Michael Msendekwa kura 122 na Mwanga Chibago kura 37.

Katika Mkoa wa Pwani wabunge watatu waliomaliza muda wao wameanguka akiwemo Dk Shukuru Kawambwa, Mbaraka Dau na Ally Ungando. Kwenye jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge aliongoza kwa kupata kura 157 akifuatiwa na Dk Kawambwa kura 90, Abdalla Buheti kura 60 na Abubakary Mlawa kura 50. Wajumbe 480 walipiga kura, mili zikiharibika.

Katika jimbo la Mafia Dau alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 95. Omary Kipanga aliongoza akiwa na kura 111 na Omary Kimbau alikuwa wa tatu. Wajumbe 258 walipiga kura huku mbili zikiharibika. Kwenye jimbo la Kibiti, Twaha Mpembenue aliongoza kwa kupata kura 275, akifuatiwa na Ungando kura 258 na Amina Mkumba kura 80. wajumbe 757 walipiga kura.

Kwenye jimbo la Kibaha Mjini, mbunge aliyemaliza muda wake, jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka aliongoza kwa kupata kura 286, akifuatiwa na Abubakari Alawi kura 88 na Mchange Mchange aliyepata kura 69. Wajumbe 523 walipiga kura kwenye mkutano huo, moja ikiharibika.

Katika jimbo la Nyasa wilayani Nyasa, msimamizi wa uchaguzi huo, Ally Haji Ramadhani alimtangaza, Stella Manyanya kuwa aliongoza kwa kupata kura 539 na kuwashinda wananchama wengine 15. Kwa mujibu Ramadhani, wanachama 764 walipiga kura, moja iliharibika.

Manyanya ni mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo hilo. Kwenye uchaguzi huo, Manyanya alifuatiwa na Cassian Njowoka aliyepata kura 76. Katika jimbo la Ngara, Ndaigaaba Ruhoro aliongoza kwa kupata kura 211 wakati mbunge aliyemaliza muda wake, Alex Gashaza alipata kura 144, na Issa Same kura 132.

Jimbo la Bukoba Vijijini, Nestory Kulinda alimtangaza mbunge aliyemaliza muda wake, Jason Rweikiza akiongoza kwa kupata kura 404. Yasir Matsawili alikuwa wa pili kwa kura 101 na Ismail Nasoro kura 43.

Kwenye jimbo la Muleba Kusini msimamizi wa uchaguzi, Hamimu Mahamudu alimtangaza Denis Kinubu kuwa ameongoza kwa kupata kura 335, Oscar Kikuyu kura 174 na Modest Rwelamula kura 79.

Mbunge aliyemaliza muda wake, Profesa Anna Tibaijuka hakugombea baada ya kuamua kupumzika. Wabunge wengine kwenye mkoa wa Kagera waliomaliza muda wao na wameanguka kwenye kura za maoni ni wa jimbo la Biharamulo Oscar Mkasa aliyepata kura 8, Dk Balozi Deodorus Kamala jimbo la Nkenge kura 24. Kwenye Jimbo la Malinyi, Antipas Mngungus aliongoza kwa kupata kura 125, alifuatiwa na Mectidios Mdaku kura 91.

Mbunge aliyemaliza muda Dk Haji Mponda amekuwa wa tatu kwa kupata kura 49. Kulikuwa na wagombea 34, wajumbe 361 walipiga kura. Mchakato wa kura za maoni jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam uliingia dosari na ikaibuka hali ya sintofahamu baada ya kubainika kuwa baadhi ya karatasi za kupigia kura zenye majina ya wagombea, kuwa na kurasa pungufu.

Mkoa wa Dar es Salaam una majimbo 10 ya uchaguzi, umekamilisha mchakato wa kura za maoni wa CCM. Kwenye jimbo la Ukonga upigaji kura za maoni ulikamilika juzi usiku Sintofahamu katika uchaguzi huo ilitokea baada ya baadhi ya fomu yenye majina ya wagombea kuwa na karatasi pungufu hivyo kusababisha malalamiko.

Kutokana na kasoro hiyo, upigaji kura ulisitishwa kwa muda ili tatizo hilo lifanyiwe kazi. Mratibu wa uchaguzi katika jimbo hilo la Ukonga, Musa Kilakala alisema kasoro hiyo ilifanyiwa kazi na kwamba wapigakura waliridhika na kuendelea kupigakura.

"Ni kweli kuna baadhi ya karatasi zilikuwa zinakosa ukurasa wa nne na wa tano ila tumechapa tena karatasi zenye majina yote ya wagombea kwa kuwa tunaamini kila mtu anastahili kupigiwa kura," alisema wakati mchakato huo ulipositishwa.

Mchakato ulikamilika saa mbili usiku na aliyekuwa Meya wa Ilala, Jerry Slaa aliongoza kwa kupata 206, Robert Masegese 118, na Mohammed Msofe kura 60. Katibu wa CCM wilaya ya Ilala, Idd Mkowa alisema, ushindi wa kura za maoni kwa wagombea hao si hatua ya mwisho kwani majina yote ya waliogombea wakiwemo waliopata kura sifuri yatapelekwa kwenye vikao vya ngazi za juu vitakavyoteua mgombea kukiwakilisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.

Alisema katika jimbo hilo, kulikuwa na wagombea 146, zilipigwa kura 552, moja ikiharibika. Katika jimbo la Kibamba upigaji kura ulikamilika saa nne usiku. Issa Mtemvu aliongoza kwa kupata kura 83, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Vick Kamata amepata kura 49 na Mwesigwa Siraji kura 36.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Chief Yaredi, jimbo hilo lilikuwa na wanachama 176 waliochukua fomu lakini waliorejesha na kupigiwa kura ni 170. Aliyekuwa mbunge jimbo la Mbagala, Issa Mangungu amekuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 65. Abdallah Chaurembo alishinda kwa kupata kura 316 na mshindi wa tatu ni Lucas Malegeli aliyepata kura 34.

Katibu wa CCM, Wilaya ya Temeke, Andrea Gwaje alisema jimbo hilo lilikuwa na wagombea waliopigiwa kura 91. Waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo walikuwa 96 ila waliorejesha ni 91. Jimbo la Mbeya vijijini, Oran Njeza aliongoza kwa kupata kura 491 akifuatiwa na Dickson Sinkwembe aliyepata kura 202 na nafasi ya tatu ni Edwald Shiwa kura 167.

Jimbo la Chunya Masache Kasaka aliongoza kwa kupata kura 460, akifuatiwa na Mbunge aliyemaliza muda wake Victor Mwambalaswa aliyepata kura 86 na nafasi ya tatu na Geofrey Mwankenja kura 84.

Jimbo la Rungwe, Saul Amon aliongoza kwa kura 404, akifuatiwa na Antony Mwantona aliyepata kura 318 na Goodluck Mwangomango kura 69. Jimbo la Kyela, Ally Mlagila aliongoza kwa kupata kura 502, akifuatiwa na Hunter Mwakifuna kura 288 na Dk Harrison Mwakyembe kura 252.

Katika jimbo la Ulanga kulikuwa na wagombea 38, zilipigwa kura 703, na 15 ziliharibika hivyo kura halali zilikuwa 688. Katibu wa CCM Wilaya ya Ulanga, Dk Sadakati Kimati alisema Salim Alaud Hasham aliongoza kwa kupata kura 219. Mbunge aliyemaliza muda wake, Goodluck Mlinga amepata kura 124, akifuatiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Furaha Lilongeli amepata kura 117.

Kwenye jimbo la Mikumi kulikuwa na wagombea 47, msimamizi wa uchaguzi, Deogratias Rutta alimtangaza Jonas Nkya kuwa ameongoza kwa kupata kura 249. Dennis Londo amekuwa wa pili kwa kupata kura 103, Said Kinyowa amekuwa wa tatu akiwa na kura 97 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilosa , Amer Mbaraka Ahamed amepata kura 83. Katika jimbo la Mlimba kulikuwa 39, Godwin Kunambi ameongoza kwa kupata kura 193, na alifungana na Rose Rwakatare aliyepata kura 193.

Pia katika uchaguzi huo Acrey Mhenga alipata kura 124 na Jane Mihanji amepata kura 14. Kwenye jimbo la Malinyi, Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Issack Kalleiya alisema kulikuwa na wagombea 34 na Antipas Mgugusi ameongoza kwa kupata kura 125.

Mecktiris Mdaku amepata kura 91, na Mbunge aliyemaliza muda Dk Haji Mponda amepata kura 47. Jimbo la Morogoro Kusini kulikuwa na wagombea 23, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogeris aliongoza kwa kupata kura 304.

Mathew Mtigumwe amepata kura 286, Zuberi Yahya Mfaume amepata kura 40. Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara alishinda katika Jimbo la Tarime Vijijini kwa kupata kura 291, akifuatiwa na Jemsi Bwire kura 135 na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eliakim Maswi alipata kura 128.

Jimbo la Tarime Mjini Jackson Ryoba Kangoye aliongoza kwa kura 126, Michael Kembaki alipata kura 64 na Martin Mwita alipata kura 20, Wakili Onyango Otieno kura 11.

Katika Jimbo la Rorya, Jafari Chege aliongoza kwa kupata kura 152 akifuatiwa na Olwaro Ganga kura 121 na Leonard Otuoma kura 52.

Imeandikwa na John Nditi (Morogoro), John Gagarini (Kibaha), Sifa Lubasi (Dodoma), Diana Deus (Bukoba), Joachim Nyambo (Mbeya).

Chanzo: habarileo.co.tz