Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge 28 wa CUF njia panda

47790 CUF+PIC

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pemba. Ruzuku, mahaba kwa Maalim Seif Sharif Hamad na shinikizo la wananchi ni miongoni mwa mambo yanayowapa wakati mgumu wabunge 28 wa CUF.

Maalim Seif, aliyekuwa katibu mkuu wa hicho, amehamia ACT-Wazalendo na kuwataka wanaomuunga mkono wamfuate, huku akiwapa fursa wabunge hao kufanya uamuzi wanaoona unafaa, akisema ni “hiari yao kumfuata sasa au kusubiri” hadi muda wao utakapomalizika.

Lakini, wakati Maalim Seif akitoa demokrasia kwa wabunge hao, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameshawatahadharisha wabunge hao kuwa “akili za kuambiwa na Maalim Seif wachanganye na zao”.

Kisiwani Pemba, wananchi wengi wanaomuunga mkono Maalim Seif wamewataka wabunge hao kumfuata kiongozi huyo ACT-Wazalendo.

Mmoja wa wananchi hao, Soud Marhoun kutoka wilayani Wete mkoani Kaskazini, alisema haoni haja ya wabunge hao kuendelea kubaki upande wa Profesa Lipumba kwa kuwa kipindi chote cha mgogoro walikuwa na Maalim Seif.

Soud alisema kuendelea kubaki CUF kutakinufaisha chama hicho kipato kwa kuwa kiasi cha fedha ambacho wabunge wanatakiwa kuchangia chama.

Taarifa zisizo rasmi zinaeleza chama hicho kila mwezi kinapata ruzuku ya kiasi cha Sh138 milioni na wabunge wanatakiwa kuchangia kila mwezi. Wabunge wa majimbo wanachangia chama Sh2 milioni na wale wa viti maalumu wanachangia Sh2.5 milioni.

Upande wa Profesa Lipumba una wabunge wanane wa viti maalumu na wawili wa majimbo, wakati wa upande wa Maalim Seif ulikuwa na wabunge 28 wakiwamo wa viti maalumu.

Soud alifananisha michango ya kila mwezi ya wabunge hao kwa CUF kuwa ni sawa na kuchangia ukandamizaji wa demokrasia nchini.

Alisema endapo wabunge hao wataamua kumfuata Maalim Seif watapata fursa tena ya kugombea kwenye majimbo yao kupitia ACT-Wazalendo na wataweza kushinda tena, hasa kisiwani Pemba.

“Wakumbuke hata Maalim Seif alikataa kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio kwa kusimamia haki yake wakati alikuwa na hakika angepata nafasi ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini yote hakujali aliamua kutoshiriki akitaka haki isimame,” alisema.

Kwa mujibu wa katiba iliyofanyiwa marekebisho baada ya CCM na CUF kufikia muafaka, mgombea urais anayeshinda ndiye anayeongoza nchi na wa pili anayepata asilimia 10 ya kura zote, anatakiwa awe Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Soud pia alikumbusha kitendo cha wawakilishi kutotetea nafasi zao katika uchaguzi wa marudio ulioitishwa baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu. “Tunapaswa kuangalia pia kuwa wawakilishi wetu walishashinda na kupewa vyeti vya ushindi, lakini waliamua kukaa pembeni na kutoshiriki tena kwenye uchaguzi wa marudio. Yote ni kuonyesha msimamo wao kwa nini wabunge nao wasiwe tayari kwa hili,’’ alisema.

Hata hivyo, katibu wa wabunge wa CUF, Juma Kombo Hamad (Wingwi, Kaskazini) alisema muda si mrefu wabunge wote watakutana na watafanya maamuzi wanayoona ni sahihi.

Alisema kwa hatua ya awali wameshaamua kumuunga mkono Maalim Seif na wao muda si mrefu watahama chama hicho na kuingia ACT-Wazalendo ili kuendeleza dhamira ya kusaka haki kwa wananchi wao.

Kombo alisema haiwezekani kiongozi wao mkuu alikata kuendelea na nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na kusimamia haki, halafu wao waendelee kuwa wabunge.

Mratibu mkuu wa CUF kisiwani Pemba, Said Ali Mbarouk alisema wabunge hao wanapaswa kujiangalia na kutafakari hatima yao.

Hata hivyo, alisema anafahamu kuwa jambo hilo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, hivyo wabunge hao watumie muda mwingi kutafakari kabla ya kufanya maamuzi yoyote yale.



Chanzo: mwananchi.co.tz