Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge 19 Chadema waanza kazi bungeni

711d50b5518a900482834b28254efe9c Wabunge 19 Chadema waanza kazi bungeni

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WABUNGE 19 wa Viti Maalumu kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walihudhuria kikao cha kwanza cha mkutano wa Pili wa Bunge la 12. Pia wabunge wanne kutoka Chama cha ACTWazalendo, walihudhuria kikao hicho kwenye ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bavicha), Halima Mdee waliapishwa Novemba 23, mwaka huu na kuibua mgogoro ndani ya chama hicho.

Wabunge hao walivuliwa uanachama baada ya viongozi wakuu wa Chadema kukana kuwatambua. Wabunge waliohudhuria bungeni jana ni Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Mdee na wenzake 18 walikata rufaa mwezi mmoja tangu walipofukuzwa katika chama licha ya kuapishwa na Spika wa Bunge ili kuitumikia nafasi hiyo. Walikata rufaa kupinga uamuzi wa kuvuliwa uanachama, utakaomaanisha kuikosa nafasi hiyo ya uwakilishi bungeni.

Chama hicho kilichelewa kuwasilisha majina ya wabunge, watakaokiwakilisha bungeni kwa nafasi ya 19 za viti maalumu kulingana na kura za wabunge chama hicho, kilizopata baada ya kususa kutokana na kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu, uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Pamoja na wabunge hao 19, wabunge wengine waliohudhuria Bunge hilo la 12 ni wabunge wanne wa ACT - Wazalendo ambao ni Khatibu Said Haji (Konde), Salum Mohamed Shafi (Chonga), Omar Ali Omar (Wete) na Khalifa Mohamed Issa wa Mtambwe. Wabunge hao waliapishwa Desemba mwaka jana, baada ya kuchelewa kuhudhuria bungeni kutokana na mgogoro uliotokana na masuala ya uchaguzi.

Wabunge wengine waliohudhuria kwa mara ya kwanza bungeni ni wabunge watano wa kuteuliwa na Rais ambao ni Humphrey Polepole, Riziki Lulida, Dk Dorothy Gwajima ambaye sasa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Chamuriho ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Profesa Shukrani Manya ambaye ni Naibu Waziri wa Madini.

Chanzo: habarileo.co.tz