Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge 16 CCM kumvaa Lowassa Monduli

15281 Pic+lowasa TanzaniaWeb

Mon, 3 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Wabunge 16 wa CCM wameweka kambi katika Jimbo la Monduli kumfanyia kampeni mgombea wa chama hicho, Julius Kalanga dhidi ya mgombea wa Chadema, Yonas Laizer ambaye kampeni zake zinaongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Kalanga aliyeshika jimbo hilo mwaka 2015 kutoka mikononi mwa Lowassa aliyelikalia tangu mwaka 1995, anawania ubunge kupitia CCM baada ya kujizulu nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema na kujiunga na chama hicho tawala Julai 31.

Tangu kuanza kwa kampeni hizo, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amekuwa bega kwa bega na Laizer, huku mashambulizi ya kisiasa yakielekezwa zaidi kwake kutokana na imani kuwa Monduli ni ngome yake.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ambao Lowassa aliachana na ubunge na kuwania urais, Kalanga akiwa mmoja wa watu waliohama naye kutoka CCM kwenda Chadema, alipitishwa na kushinda kiti hicho.

Mkakati wa wabunge CCM

Wakizungumza jana katika mkutano wa kampeni, baadhi ya wabunge wa CCM ambao tayari wamefika na kuanza kupanda jukwaani walisema hawataondoka Monduli hadi wahakikishe Kalanga anatangazwa mshindi.

Mbunge wa Ngorongoro na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha alisema idadi ya wabunge watakaoshiriki katika uchaguzi huo ni 16.

Alisema uchaguzi huo wa Monduli unarudiwa kutokana na wananchi kukosea mtihani wa mwaka 2015.

“Sasa tumekuja kwenu mfanye marekebisho ya mtihani wa mwaka 2015, tumemleta tena Kalanga akitoka chama ambacho hakina ilani ya kuwaletea maendeleo hii ni fursa ya kufanya masahihisho,” alisema.

Ole Nasha ambaye ndiye meneja kampeni, alisema Kalanga ndiye chaguo sahihi kwa wana Monduli.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda alisema Kalanga ni mchezaji mzuri wa kufunga magoli na wanamtaka afunge magoli, kwa sababu ni mchezaji mwenye sifa na viwango vyote vinavyostahili.

“Hivi inakuwaje mnakuwa na timu hata ikicheza Ndondo Cup haishindi,” alisema.

Alisema Monduli walianza kuona mambo mabaya baada ya kumchukua mchezaji mzuri kumpeleka kwenye timu mbovu.

“Sasa washangiliaji ni nyie, mchezaji ni wenu, hivyo fungeni magoli ili mfurahie ushindi sababu mna mchezaji bora katika timu nzuri,” alisema.

Mbunge wa Kondoa Mjini, Edwin Sanda alisema, “Yote yaliyofanyika Monduli yamefanyika ndani ya CCM, hivyo Rais anahitaji watu wa kumsaidia katika kuleta maendeleo, tuleteeni Kalanga akasaidiane na Rais (John) Magufuli katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Monduli na Mto wa Mbu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige aliwaomba wana Monduli wawaletee mbunge ambaye atatatua kero za wananchi akisema upinzani kazi yao ni kutoka nje bungeni kwa kuwa hawapendi maendeleo.

“Kina mama msiniangushe, najua mnahitaji mikopo, hivyo mchagueni Kalanga kwa ajili ya maendeleo ya CCM,” alisema.

Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel ambaye awali alikuwa Chadema akajiuzulu na kuchaguliwa tena, alisema waliamini wakiwa katika chama hicho cha upinzani kuwa wataweza kuzungumzia matatizo ya wananchi lakini walijikuta kwenye genge lisilofaa.

Alisema Rais Magufuli ni chuma cha mkoloni na amenyoosha mambo mengi katika nchi.

Alisema amekwenda CCM ili kuleta maendeleo na kwamba chama hicho kimeleta mabadiliko ambayo Chadema walikuwa wakiyataka hapo awali.

“Ndugu zangu msipoteze bahati hii mchagueni Kalanga,” alisema.Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma alisema Kalanga ndio suluhu ya shida za Monduli huku akimponda Lowassa kuwa amekwisha na hawezi tena kuleta maendeleo.

“Mchagueni Kalanga kama kweli mnataka maendeleo hao ‘peoples’ (Chadema) wanawapotezea muda,” alisema.

Wabunge Jiitu Son wa Babati Vijijini na Dk Stephen Kiruswa wa Longido waliwataka wananchi kutopotoshwa katika uchaguzi huo kwani Kalanga ndiye chaguo sahihi.

Mbunge mwingine, Ester Mahawe aliwataka wakazi wa eneo la Makuyuni kumchagua Kalanga ili waepukane na kuchangishwa michango isiyo na tija inayofanywa na viongozi wa Chadema.

Chanzo: mwananchi.co.tz