Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimeviibua vyama vingine vya siasa baada ya kumuomba Rais John Magufuli aruhusu mikutano ya hadhara ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Mikutano hiyo ilipigwa marufuku mwaka 2016, miezi michache baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, kwa maelezo kuwa siasa hufanywa wakati wa uchaguzi.
Viongozi walioshinda katika Uchaguzi Mkuu ndio walioruhusiwa kuitisha mikutano katika maeneo yao, lakini amri hiyo imekuwa ikipingwa na viongozi wa kisiasa ambao wanasema inakiuka Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Viongozi hao pia wanalilaumu Jeshi la Polisi kwa kutosimamia vyema amri hiyo kutokana na kuwabana wapinzani pekee.
Huku uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa ukipangwa kufanyika Oktoba, CUF ilitoa ombi hilo kwa waandishi wa habari jana na mara moja vyama vingine vikaiunga mkono ambavyo ni Chadema, ACT-Wazalendo, Chaumma, NCCR-Mageuzi huku Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Uhusiano wa Kimataifa), Kanali Ngemela Lubinga akisema uchaguzi ukikaribia mikutano hiyo itaruhusiwa.
“Tunaiomba Serikali kutoa tamko la kuruhusu mikutano ya hadhara wakati huu wa maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema Salvatory Magafu, mkurugenzi wa sheria na haki za binadamu wa CUF, alipozungumza na waandishi wa habari.
Pia Soma
- Chama cha CCM kiyafanyie kazi haya haraka kabla ya 2020
- Ndege iliyoanguka Tabora ilitua bila taarifa, kutozwa faini
- USHAURI WA DAKTARI: Kutokwa uchafu katika chuchu
“Tunamuomba Rais John Magufuli atoe tamko la kuruhusu mikutano ya hadhara kwa kuwa alipopiga marufuku aliahidi kuruhusu kipindi cha uchaguzi hivyo huu ni muda muafaka,” alisema Magafu.
Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumapili Agosti 4, 2019