Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vyalia zuio mikutano

39213 Pic+sakaya Vyama vyalia zuio mikutano

Mon, 1 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

VYAMA vya upinzani nchini vimesema kuwa kuendelea kwa zuio la mikutano ya kisiasa la tangu mwaka 2015, kunawaathiri kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hali hii imeendelea kuwapo ikiwa imebaki miezi mitano kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, mbunge na madiwani unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Wakizungumza na Nipashe, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya na Naibu Katibu Mkuu wa Uenezi, Habari na Mahusiano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Janeth Rithe na Ofisa wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene.

Walisema msingi wa vyama vya siasa ni mikutano, lakini kwa muda mrefu haifanyiki na sasa ni mwaka wa uchaguzi na bado haijaruhusiwa.

KAULI YA CUF

Sakaya alisema matarajio ya vyama vingi ilikuwa ni kuondolewa kwa zuio hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu ili kuviwezesha vyama kufanya kazi zao bila usumbufu, lakini hali imekuwa tofauti.

“Tuliambiwa mikutano inazuiwa ili watu wafanye kazi za maendeleo, huu ni mwaka wa uchaguzi tulitarajia vyama vingeruhusiwa kuendelea na mikutano kwa kuzingatia vyama ndiyo wadau wakubwa, ndivyo vyenye watu na huwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila mikutano, lakini hadi sasa zuio liko pale pale,” alisema.

Aidha, alisema wakati kukiwa na zuio hilo bado wameendelea kuitwa kwenye mambo mbalimbali ya maandalizi ya uchaguzi mkuu kama hivi karibuni waliitwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kupitisha maadili ya uchaguzi, na Msajili wa Vyama vya Siasa alitaka ratiba zao, lakini hakukuwa na ufafanuzi wowote kuhusu zuio linalovikabili vyama hivyo kwa sasa.

CHADEMA YANENA

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema kuendelea kwa zuio hilo ni kiashiria kibaya cha demokrasia kwa kuwa inakandamiza haki za kikatiba na sheria.

Kwa mujibu wa Makene, ushindani kwenye majukwaa baina ya chama kilichopo madarakani na upinzani ni mgumu, hivyo kuamua kuzuia mikutano.

“Ni moja ya jambo ambalo limekwaza sana na linasababisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa sehemu ya kufanya maamuzi.”

ACT-Wazalendo

Naye Rithe wa ACT alisema vyama vya upinzani vimathirika sana kwa kutokufanya mikutano ya kisiasa kwa kuwa shughuli zao zinahusisha kukutana ambako kilipigwa marufuku mwaka 2015.

“Licha ya kwamba ni haki yetu kukutana kwa mujibu wa katiba, lakini hatuwezi kufanya hivyo kutokana na zuio lililopo kwa sasa,” alisema.

Alisema: “Kwa miaka mitano vyama vya upinzani havijafanya mikutano, lakini tumeona wenzetu wakiendelea na shughuli za siasa bila katazo lolote, hii si sawa na hadi sasa kupo kimya licha ya kwamba imebaki miezi mitano kufikia uchaguzi mkuu.”

ZUIO LA MIKUSANYIKO

Kuhusu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Fransis Mutungi, kuvitaka vyama kuwasilisha ratiba zake kuelekea uchaguzi mkuu ikiwa ni kwa mujibu wa sheria, Sakaya alisema:

“Tulimjibu msajili wa barua yake tukimuuliza suala la kuzuiwa kwa mikusanyiko kutokana na janga la corona, je, tunakwendaje na suala hili lakini hadi sasa hakuna majibu.”

Naibu Katibu Mkuu huyo ambaye ni Mbunge wa Kaliua, alisema kumekuwa na sitofahamu kwa kuwa CUF ilipaswa kuanza mchakato wa kura za maoni mwanzoni wa mwezi huu, lakini hadi sasa hakua jibu lolote.

“Kuzuiliwa kwa mikusanyiko kwa sababu ya janga la corona kumethiri shughuli zetu za kisiasa, hatuna kibali cha mikutano tumemwandikia msajili hajajibu, tunashindwa kufanya kura za maoni ambazo hukusanya watu wengi kwa wakati mmoja,” alisema.

Kwa mujibu wa Sakaya, mikutano yao huwa na wajumbe 100 hadi 300 kwa ngazi ya kata, wilaya ni 600 hadi 1,000 kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea, kwa mgombea urais ni zaidi ya wajumbe 1,200.

Alisema kupitia mikutano hiyo ndiyo huamua na kupitisha wagombea, na kwamba bila mikutano huwezi kuamua kwa kuwa itakuwa ni mwanzo wa kuua chama, kwa kuwa lazima wamchague mgombea kwa kupiga kura, na wanapata kigugumizi kujua hali itakuwaje iwapo serikali itaendeleza ukimya.

“Tuna zuio la mikutano ya hadhara na sasa tuna zuio la mikusanyiko, huwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila kura ya maoni, utagawa wanachama na atakimbia, mahali kuna agomba saba hadi 10 lazima wapigiwe kura,” alisema.

Alisema CUF ilitaka kumaliza suala la kura za maoni mwishoni mwa mwezi huu, ili kuwa na muda wa kutosha kutibu majeraha ya uchaguzi wa ndani, lakini kwa sasa hajajua la kufanya kwa kuwa hakuna uwezekano wa mikutano ya mtandaoni.

Naye Rithe alisema wameshajibu barua ya msajili na itapelekwa leo na kwamba watu wametangaza nia na hatua inayofuata ni vikao ndani ya chama ambalo litaanza baada ya Bunge kuvunjwa Juni 19, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live