Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vyalia rafu Mtolea kupita bila kupingwa Temeke

32844 Pic+vyama Abdallah Mtolea

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Abdallah Mtolea wa CCM kutangazwa kupita bila kupingwa katika ubunge Jimbo la Temeke, baadhi ya vyama vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo vimelia kuchezewa rafu na msimamizi wa uchaguzi.

Juzi, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Temeke, Lusibilo Mwakabibi alimtangaza Mtolea kushinda kwa maelezo kuwa wagombea wengine waliokuwa wamechukua fomu kuwania nafasi hiyo wamekosa sifa.

Katika hati ya kuchaguliwa kuwa mbunge ambayo gazeti hili limeiona inaeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 81 (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 amechaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi uliofanyika jana (juzi, Desemba 20).

Hatua hiyo ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza Mtolea imewaibua viongozi wa vyama vilivyosimamisha wagombea baadhi yao wakidai kuwa mamlaka hazitaki uchaguzi ufanyike na jambo hilo siyo mara ya kwanza kutokea.

“Inavyoelekea hawataki uchaguzi ufanyike, ilitokea kule Jimbo la Korogwe Vijijini, leo Dar es Salaam. Hivi kweli vyama vyote vya upinzani vilivyosimamisha wagombea vinaweza kushindwa kujaza fomu ya maadili kisheria,” alihoji Abdul Kambaya, mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF.

“Nyie mnajua ni Mtolea, lakini kuna diwani wa Keko na yeye amepita bila kupingwa. Tutaendelea kujenga hoja kuhusu sintohamu hii ili Watanzania wajue ukweli.”

Katibu Mkuu wa NRA, Hassan Kisabya alisema walifuata taratibu zote katika mchakato huo na wakati wa kurudisha fomu za mgombea msimamizi wa uchaguzi hawakumkuta badala yake walitakiwa kumsubiri.

“Mgombea wetu alijaza fomu zote isipokuwa ile namba 10 ya maadili ya kisheria ambayo tulielezwa kuwa hatuwezi kuisaini bila msimamizi wa uchaguzi kuwepo. Tulifika saa tatu asubuhi lakini hadi saa 10:20 jioni ndipo mkurugenzi wa uchaguzi akatokea na tukaelezwa hakuna jinsi muda umeisha,” alisema Kisabya.

“Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi maana tatizo lililopo hapa ni mfumo. Tunaambiwa kitu hiki hakiwezekani hadi awepo msimamizi mkuu, sasa akichelewa au asipokuja itakuwaje?”

Katibu mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Lai alisema hajui kwa undani kilichokea, lakini alielezwa na mgombea wao kuwa fomu namba 10 ndiyo iliyowakosesha sifa.

Mwananchi lilipomtafuta Mwakabibi kutoa ufafanuzi alitaka watafutwe waandishi wengine au wale wa manispaa.

“Watafute waandishi wenzako au manispaa wakueleze,” alisema.

Akizungumzia mchakato ulivyokuwa juzi, Mtolea ambaye awali alikuwa mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF na kuhamia CCM ambako alipitishwa tena kuwania ubunge alisema, “Tuliojitokeza kugombea Temeke tulikuwa 14, wanne hawakurejesha fomu na tisa waliorejesha zilionekana kuwa na kasoro.”

Baadhi ya wanasheria waliozungumzia uwezo wa kisheria wa msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mgombea kushinda kabla ya tarehe ya uchaguzi walitaja mazingira na sababu zinazompa nguvu.

“Endapo mgombea amebaki peke yake au amepita bila kupingwa anakabidhiwa hati na kutangazwa mshindi na msimamizi wa uchaguzi,” alisema wakili wa kujitegemea Dk Onesmo Kyauke.

Wakili Rainery Songea alisema mtu anaweza kutangazwa kuwa mshindi iwapo hakuna mapingamizi miongoni mwa wagombea wenzake, lakini kama yapo msimamizi analazimika kumtangaza tarehe husika ya uchaguzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz