Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya upinzani vifanyie kazi haya kabla ya 2020

72859 Upinznai+pic

Mon, 26 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kiushindani, siasa ni hesabu. Sayansi ya siasa inatuaminisha kwamba bila hesabu, hakuna chama au mgombea anayeshinda dhidi ya mpinzani wake kwa miujiza.

Hesabu hizo zinaweza kufanyika kupitia hatua mbalimbali ikiwamo matumizi ya tafiti za awali kuhusu maoni ya wananchi. Udhaifu au ubora wa kazi zinazofanywa na serikali iliyopo madarakani kwa wakati huo ni mtaji wa upinzani lakini itategemea na utayari wa upinzani.

Uchambuzi wa hali ya siasa za upinzani ndani ya miaka minne sasa nchini imeonekana kuwagawa Watanzania, wengine wakiamini kuna anguko kubwa la upinzani kutokana na utendaji wa Rais John Magufuli. Wengine wanahofia zuio la mikutano ya hadhara, ndani.

Profesa Mohamed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya siasa na utawala bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaibua matumaini akisema pamoja na mazingira hayo, ni mapema sana kutabiri ‘mauti’ ya vyama vya upinzani katika uchaguzi huo kutokana na tabia za wapiga kura.

Profesa Bakari anasema matukio yatakayotokea kabla ya 2020 yatatoa ishara za kuamua hatma ya ushindani katika uchaguzi huo.

Ikiwa ni takribani mwaka mmoja umebakia kabla ya uchaguzi huo, vyama vya upinzani vinalazimika kufanyia kazi haraka maeneo sita endapo inahitaji kuwa imara kiushindani ili kupata kibali cha kuongoza Watanzania kwa ngazi mbalimbali.

Pia Soma

Maeneo hayo ya kiutafiti ni pamoja na kuhakikisha vinaeleza hatma ya ushirika wa vyama vyao, uchambuzi wa wagombea, wagombea ngazi ya chini, sera zitakazouzika, uwezo wa kifedha ili kukabiliana na changamoto za rufaa, gharama za mawakili na kujinadi vijijini.

Ushirika wa vyama

Katika uchaguzi wa 2015, vyama vinane kati ya 11 viliungana chini ya ubatizo wa Ukawa na kumsimamisha mgombea wa urais, Edward Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97 huku Dk John Magufuli wa CCM akipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47.

Vyama hivyo ni Chadema, Cuf, NCCR Mageuzi na NLD. Uchaguzi huo ulikuwa na matokeo chanya yaliyoweka historia ya kura za urais na idadi ya wawakilishi.

Hata hivyo, haijafahamika bado endapo Ukawa itazaliwa upya au kutakuwa na ubatizo wa sura nyingine ya usharika wa vyama hivyo. Tayari kuna vyama kumi vimeonekana kuendesha harakati za kupinga madai ya ukandamizaji wa demokrasia nchini.

Mwalimu Nderakindo Kessy, Katibu wa Mambo ya nje wa NCCR Mageuzi anasema usharika hauepukiki na muda uliobaki unatosha kutabiri mazingira ya kisiasa kabla ya uchaguzi huo.

“Mazingira ndiyo yalizalisha ukawa, sasa mazingira ni tofauti. Nia ya ushirikiano ipo lakini hatujui mazingira yatakavyojitokeza hapo baadaye, tusubiri tuone,” anasema Nderakindo.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Temu anasema kura za wagombea wa upinzani ndani jimbo moja zilikuwa nyingi kuliko kura za mgombea mmoja wa CCM, hivyo endapo

wapinzani wataachiana maeneo, watachukua majimbo mengi badala ya kutawanya nguvu za upinzani.

Uchambuzi wa wagombea

Wimbi la wabunge zaidi ya kumi, madiwani zaidi ya 150 wa vyama vya upinzani, wengi wakitokea Chadema walirejea au kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM). Ni upepo ulioshtua wafuasi wengi wa vyama hivyo hususani chama kikuu cha upinzani Chadema.

Upepo huo haukupata sababu moja. CCM walidai ni juhudi za kuunga mkono utendaji kazi wa Rais John Magufuli na upinzani wakiamini ni mkakati uliotumia nguvu ya fedha na ahadi ya kupewa uongozi kwa wale watakaojiunga au kurejea CCM.

Wachambuzi wa duru za kisiasa wanasema hatua hiyo ilichagizwa na makosa ya vyama vya upinzani kusimamisha wagombea wenye maslahi binafsi zaidi, ambao hawakujengewa misingi ya kiitikadi au Imani ya chama, dosari aliyokiri Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicenti Mashinji.

Wafuasi wa vyama hivyo wanatamani kuona dosari hiyo ikipatiwa ikifanyiwa kazi kupitia uchambuzi wa wagombea wanaoamini na kuishi itikadi ya chama hicho kabla ya uchaguzi ujao.

Kusimamisha wagombea wengi chini

Mbali na uchambuzi wa wagombea, suala la uwakilishi ngazi ya chini ndiyo mtaji mkubwa wa chama kuingia Ikulu. Matokeo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, yatatoa mwelekeo wa vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao.

Tathmini inaonyesha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, CCM kilipata ushindi wenyeviti 9,406 huku vijiji 3,211 vikibakia vyama vya upinzani, sawa na asilimia 34, ambao baadhi walishahamia CCM, jambo linalotishia nguvu ya upinzani.

Katika maeneo walikoshinda upinzani ilisaidia kuwa na nguvu ya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambao pia waliongeza idadi ya wabunge na madiwani huku wakipata kura za kihistoria kwa mgombea wao wa urais, Edward Lowassa.

Endapo vyama hivyo vitasimamisha wagombea wengi uchaguzi wa serikali za mitaa, wenye sifa za kushindana licha ya madai ya kuwapo tuhuma za hujuma za kisiasa, itakuwa mtaji wa 2020.

Kufikia wengi vijijini

Hadi sasa, CCM ndiyo chama kilichofanikiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi maeneo ya vijijini. Lakini bado haitafsiri waishio maeneo hayo ni wanachama au wafuasi wa kudumu wa CCM.

Vyama vinavyofuata baada ya CCM ni Chadema, CUF, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi kwa mujibu wa takwimu za matokeo ya uchaguzi yanayoonyesha utofauti huo kwa Tanzania bara na visiwani.

Dk Mashinji anasema hali siyo nzuri katika njia kadhaa za ujenzi wa chama. “Kwa ngazi ya chini, tunajivunia kufikia Watanzania katika asilimia 68 ya vitongoji( misingi). Lakini, viongozi wetu katika maeneo hayo wanabandikiwa kesi na kukamatwa na Polisi,” anasema Dk Mashinji.

Taratibu za uchaguzi

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, vyama vya upinzani vilipoteza nafasi ya majimbo na kata kwa dosari za umakini katika kuzingatia taratibu za uchaguzi. Hata hivyo, baadhi ya wagombea walilalamika kuwa ni hujuma za kisiasa zilizofanywa na washindani wao.

Katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Temu anasema ushahidi unaonyesha wagombea wa upinzani hufanyiwa figisu za kisiasa ili kutoa mwanya wa mgombea wa chama kingine kupata ushindi, akiahidi kuwapo kwa uchaguzi ujao umakini zaidi katika uchaguzi ujao.

“Kuna ushahidi wa maeneo mengi yanayoonyesha mgombea kuwekewa zengwe, asiwe sehemu ya ushiriki huo. Kinachotakiwa uchaguzi ujao vyama vifanye kazi pamoja, pia mamlaka zinazohusika na uchaguzi, zisimamie uchaguzi huo kwa haki,” anasema Dorothy.

Chanzo: mwananchi.co.tz