Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya upinzani njia panda kushiriki chaguzi za marudio

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitangaza Desemba 2, kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa majimbo ya Serengeti, Simanjiro na kata 21 Tanzania Bara, vyama vya upinzani vipo njia panda kushiriki uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya wabunge wa majimbo hayo, Marwa Chacha wa Serengeti na James Ole Millya wa Simanjiro, kujiuzulu na kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Akilizungumzia suala hilo jana alipozungumza na Mwananchi, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema chama chake kitaendelea kushiriki chaguzi hizo ili kuziba pengo la kuzuiliwa kwa siasa za majukwaani.

“Kwenye kampeni za chaguzi hizi tunaona ndiko tunapata mahali pa kuzungumzia,” alisema Shaibu.

Alisema kushiriki kampeni za chaguzi hizo hasa zilizopita, kumewasaidia kuongeza idadi ya wanachama na kunadi sera zao.

“Msimamo wa chama ni kuendelea kushiriki, kamati ya uchaguzi itakutana ndani ya wiki hii kufanya tathmini ya uchaguzi wa Liwale. Kama itaona kuna tatizo au hali haikuwa nzuri, itaifahamisha kamati kuu ambayo inaweza kufanya uamuzi mgumu, hivyo tusubiri ndani ya wiki hii tutapata jibu la moja kwa moja,” alisema Shaibu.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Abdul Kambaya alisema wanasubiri tathmini ya Baraza Kuu ili kujiridhisha kama wanaweza kushiriki au la.

“Kwa yaliyotokea Liwale, hatuwezi kusema wala kufanya lolote kuhusu hizo chaguzi zilizotangazwa hadi baraza kuu likae na kutoa tathmini ambayo itaamua tunaingia au hatuingii,” alisema Kambaya.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema msimamo wa Chadema wa kutoshiriki chaguzi ndogo zote bado uko palepale. Alisema kwa kuwa Tume imetangaza jana tarehe ya uchaguzi, hawajakaa kikao chochote kujadili suala hilo.

“Kama uamuzi wa awali utatenguliwa au utabaki kama ulivyo, umma utafahamishwa, lakini kwa sasa hakuna mabadiliko,” alisema Mrema.

Akieleza kuhusu chaguzi hizo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Oktoba 28 hadi Novemba 3.

“Uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 3, kampeni za uchaguzi zitaanza Novemba 4 hadi Desemba Mosi ikifuatiwa na uchaguzi utakaofanyika Desemba 2,” alisema Jaji Kaijage.

Alizitaja kata zitakazoshiriki uchaguzi huo kuwa ni Ilboru, Mlanfarini na Oldonyosambu (Wilaya ya Arusha), Engutoto na Olasiti (Manispaa ya Arusha), Hazina (Manispaa ya Dodoma), Chinugulu (Wilaya ya Chamwino), Kasharu, Nyakimbili, Kishongo (Wilaya ya Bukoba), Chonyonyo, Ihanda (Wilaya ya Karagwe).

Nyingine ni Muhindawa, Mnanila (Wilaya ya Buhigwe), Mnerongongo (Wilaya ya Nachingwea) Ngarenairobi (Siha), Kyanyari (Butiama), Namilembe (Ukerewe), Lukanga, Beta (Mkuranga) na Chikola (Wilaya ya Manyoni).

Chanzo: mwananchi.co.tz