Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya siasa kutandaza mikeka

Vyama Vya Siasa Ruzuku Vyama vya siasa kutandaza mikeka

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kila chenye mwanzo kina mwisho, yanadhihirika kwa sasa maana yale yaliyojiri katika ulingo wa siasa kwa miaka saba yamebadilika, ni ruhusa ya mikutano ya kisiasa.

Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iliyozuiliwa imerejeshwa kuashiria ‘zuio’ limefikia mwisho, kwa hali hiyo, ‘hakuna lisilowezekana chini ya jua’ hivyo tumshukuru Mungu kwa yote na kuiombea nchi yetu.

Vyama vya siasa vilikuwa vimekunja ‘mikeka’ sasa vinaitandaza rasmi ni hatua inayowezesha kutekeleza mambo mema kwa taifa hili kwa amani, maridhiano na upendo.

Aidha, ni jambo la kufurahisha kuwepo na utashi mkubwa wa kisiasa wa namna ambayo Tanzania imezingatia ili kuimarisha demokrasia na kwa maslahi ya wote.

Kwa muda mrefu CCM imeongoza nchi uwepo wa vyama vingi katika siasa za Tanzania ni dalili tosha kwamba haitatawala au kuongoza nchi au dola milele.

Tusemeje juu ya hali hiyo? Ni kwamba sasa kumekucha na dalili za kuashiria kwamba mzinga uliosheheni nyuki ulikuwa umefunikwa sasa mfuniko umeondolewa nyuki wametawanyika kila mahali wakitafuta chavua ili kutengeneza asali iliyosheheni utamu.

Lipo swali 2025 wananchi watarajie kupata asali iliyo-tamu zaidi au kitu gani baada ya nyuki kuondoka kwenye mzinga? Hapa ndipo, ilipojificha siri ya mafanikio kwa kila chama cha siasa.

Wakati Tanganyika au Tanzania Bara, inapata Uhuru Desemba 9, 1961 kilikuwepo Chama cha Tanganyika African National Union (TAN) wakati huo Zanzibar ilikuwapo na Afro-Shiraz na hatimaye kujitawala baada ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Haikuchukua muda mrefu, Serikali ya ‘Tanganyika’ iliyokuwa inaongozwa na TANU na ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Afro-Shiraz zikaungana Aprili 26, 1964 na kuanzisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, kukawepo utawala wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ikabaki na utawala wake wa ndani chini ya Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikawa inasimamia shughuli zote zilizokubaliwa na pande mbili kuwa za Muungano; lakini pia kushughulikia masuala yote yanayohusu iliyokuwa Tanganyika.

Hata hivyo, vyama hivyo viwili TANU na Afro-Shiraz, viliendelea kusimamia serikali hadi ilipozaliwa CCM Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa.

Baada ya hapo sera na siasa, vikawa vyombo vinavyosimamiwa na chama kimoja CCM Bara na Zanzibar hadi tulipoingia mfumo wa vyama vingi Aprili 28, 1992, ni baada ya kuridhia mfumo huo kichama na kisheria.

KUJISAHAU

Kwa upande wa CCM, wakati mwingine, kumekuwepo na kujisahau na mambo yakawa hayaendi ipasavyo. Pengine, Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, mpaka kufikia uamzi huu wa kuruhusu mikutano ya vyama pinzani katika ulingo wa siasa, inawezekana hafurahishwi na hali hiyo.

Ili chama anachokiongoza kiwe msatari wa mbele, kinahitaji kuamshwa ili kutimiza wajibu wake ipasavyo kinyume chake kitajilaumu chenywe.

Kufika 2025 CCM itakuwa ina takriban miaka 50 huu siyo umri mdogo. Watanzania waliozaliwa wakati huo sasa ni watu wazima, inawezekana baadhi yao ni viongozi ndani ya chama.

Hivyo, ni kipindi kirefu kinatosha kwa chama kujipima na kujitathmini ipasavyo, maana ni takribani miongo mitatu tangu Tanzania iingie mfumo wa vyama vingi; kwa kipindi hicho lipo swali watu wamefanikisha na kujifunza nini?

TUNAJIFUNZA NINI?

Hakuna majibu kwa swali hili lakini ni vizuri Watanzania wakatafakari kwa kina kuhusu jambo hilo muhimu.

Yawezekana moja ya mafanikio ni uwepo wa demokrasia na uhuru wa kufanya mambo. Zaidi ya hapo ni kujiuliza demokrasia maana yake nini, inaanzia na kuishia wapi au mambo ni hivyohivyo ili mradi baadhi ya watu wafurahi na mambo yaende? Tena hakuna uvunjaji wa sheria za nchi na kanuni zake?

Itakumbukwa ni zaidi ya miaka 60 tangu Uhuru ni kipindi ambacho nchi kama China sasa ni mataifa yenye nguvu kiuchumi na tishio duniani.

Historia inaonyesha kuwa wakati Tanzania inapata uhuru Wachina hawakuwa na nguvu kama walizonazo sasa je, wamefanyaje au ni mbinu gani walizotumia hadi kufikia hapo walipo?

Ni nguvu ya demokrasia au kuna ‘siri’ ya mafanikio yao zaidi ya dhana hiyo? Kwa upande wa Tanzania ndani ya kipindi hicho cha miaka 60 bado tunahangaikia huduma muhimu za kijamii ukiachilia mbali kuhangaikia uchumi na ujenzi wa viwanda.

TUMESHINDA VITA?

Wakati tumepata uhuru tulitangaza vita dhidi ya maadui maradhi, ujinga na umaskini. Hata hivyo, ukawa msisitizo kuwa ili kupambana sawasawa tunahitaji miundombinu imara ya barabara na kuwa na vyanzo vya uhakika vya nishati pamoja na kuendeleza kilimo chetu ili tupate uhakika wa kupata mazao ya chakula na biashara.

Katika vita ya kuondoa maadui hao watatu pia inaendana na kuongeza nguvu katika huduma za maji, elimu na afya. Hivyo kujenga na kuweka miundombinu imara katika sekta hizo hakukwepeki pamoja na kuwepo siasa safi na uongozi bora, pamoja na rasilimali ardhi na watu,wataalam na juhudi za kutosha.

Tukijitathmini tulikotoka, tulipo na tunakoelekea naweza kusema tumethubutu kwa kiasi fulani lakini kazi bado kubwa. Kusema kweli, kama siyo vita vya ‘Iddi Amini wa Uganda’ na kusababisha taifa kutumia rasilimali au fedha nyingi, vifaa na nguvukazi bila kutarajia, pengine Tanzania iungekuwa imefanya mengi zaidi.

Miaka ya 1970 ilikuwa lijengwe bwawa-kubwa la kuzalisha umeme kwenye eneo la ‘Stigler’s Gorge’, Mto Rufiji. Hata hivyo, kutokana na athari za kivita katika uchumi ikawa imeshindikana.

Pamoja na hayo baada ya vita Tanzania ilielekeza nguvu zake katika ‘ukombozi wa mataifa’ mengine ya Africa yaliyokuwa chini ya tawala za kibeberu. Kwa hali hiyo ikawa imepungukiwa uwezo wa kushughulikia masuala ya ndani ya nchi ikiwemo kupambana na maadui waliokuwa wametangazwa rasimi kitaifa.

TUANZE SASA

Kiuhalisia huduma za kijamii na masuala ya kiuchumi bado ni mahangaiko makubwa. Kwa mtazamo huo, CCM upinzani kuweni makini katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo muhimu ya kuwaletea maendeleo-endelevu wote haraka iwezekanavyo.

Malumbano ya kisiasa na kisera yalenge kuinua hali za maisha kwa wote na isiwe kuwaneemesha wachache wakati walio wengi wanateseka ndani ya nchi yao. Vyama pinzani visiwe ni vya kulaumu na kulalamika bali vije na ‘hoja za msingi’ nini kifanyike au kitakachofanyika kwa lengo la kutumia rasilimali kwa faida ya wote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live