Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya siasa kujadili Muswada

33915 Pic+vyama Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vyama vya siasa nchini vitakutana kwa siku mbili Unguja, Zanzibar kujadiliana masuala mbalimbali ikiwamo Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambao umeibua mvutano.

Mvutano huo unatokana na kulalamikiwa na baadhi ya vyama vya upinzani vikidai endapo ukipitishwa kuwa sheria utafuta au kukandamiza demokrasia hivyo kutaka kufanyika kwa kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa ili kuujadili kwa kina.

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ilisema kikao hicho kilichokuwa kifanyike Desemba 21 na 22, sasa kitafanyika Januari 11 na 12.

Mbali na kujadili muswada huo, wajumbe watafanya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa baraza hilo pamoja na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu baraza hilo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Elimu kwa Umma wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Mnanka ilisema kikao cha kamati ya uongozi kitafanyika Januari 8 kwa ajili ya maandalizi ya baraza hilo.

“Kwa kuwa wagombea karibu wote wamepita bila kupingwa, mkuu wa Sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda wameshauriana na kukubaliana ni vyema kikao kifanyike mapema.”

“Hatua hiyo itawezesha baraza kuandaa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na kuyawasilisha katika kamati husika ya Bunge inayoanza shughuli zake Januari 14,” alisema.

Kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kitatanguliwa na semina kwa wajumbe wa baraza hilo kuhusu utaratibu wa kutunga sheria itakayotolewa na Ofisi ya Bunge la Tanzania.

Alisema kwamba semina hiyo itafanyika Januari 9 katika ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge Zanzibar zilizopo eneo la Tunguu.

Katika siku za hivi karibuni vyama vya upinzani vimekuwa vikishinikiza kufanyika kikao cha baraza hilo ili pamoja na mambo mengine kujadili Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambao wamekuwa wakiulalamikia.



Chanzo: mwananchi.co.tz