Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vizingatie haki ya wanawake katika uongozi

6fa26bedf4ccdc87b6713d542d83b889 Vyama vizingatie haki ya wanawake katika uongozi

Thu, 25 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“SIKUFANYA kampeni za majukwaani, bali kwa kufikia watu wengi walipo na huko swali kubwa nililoulizwa mara kwa mara ni kuwa, nikichaguliwa kuwa rais, nitawezaje kutumikia mume, familia na serikali maana hiyo ni nafasi kubwa na kuna kuhudumia familia wakiwamo watoto, kumpikia na kumhudumia mume, kumfulia, kupiga pasi na kadhalika…”

Amenukuliwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Queen Sendiga alipozungumza na HabariLEO baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.

Queen alikuwa mmoja kati ya wanawake wawili waliogombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi huo akikiwakilisha chama chake cha ADC.

Je, alikuwa akijibu nini? “Niliwajibu kwa mfano kuwa, tangu mwaka 2015 Rais John Magufuli alipoonesha ujasiri, tuna kiongozi wa juu ambaye ni Makamu wa Rais; Samia Suluhu; huyu ni mwanamke; tazama anavyochapa kazi ya maana na kwa ufanisi mkubwa, lakini hajawahi kulalamikiwa na mumewe kwamba hahudumii familia kama mama.”

Jumatano iliyopita, gazeti hili lilikuwa na makala iliyomnukuu Diwani wa Kata ya Mwigobero katika Manispaa ya Musoma ambaye ni diwani pekee mwanamke wa kuchaguliwa katika manispaa hiyo, Mariam Jackson, akisema kuwa, katika kampeni zake mwaka jana, washindani wake walijaribu kumfanyia kampeni za kibaguzi kwa misingi ya jinsia.

Akasema: “Walikuwa wanasema eti mimi ni ‘mkamwana’ katika kata hiyo, nitaongozaje; yaani eti mimi nimeolewa tu kuja hapo, si mzawa maana nimezaliwa katika Kijiji cha Masinki wilayani Serengeti…”

Hata hivyo, Mariam anasema: “Wananchi walijali uadilifu na uchapakazi wanaoujua kwangu, wakapuuza kejeli na ubaguzi huo na kunichagua.”

Watu mbalimbali wanasema hayo ni miongoni mwa visingizio wanavyotumia wanaume na baadhi ya wanawake “waliomeza sumu” ya ubaguzi wa kijinsia na “kuabudu” mfumo dume ili kuwapora wanawake haki ya ushiriki kamilifu katika nafasi za siasa na uongozi zikiwamo za ubunge na udiwani.

Mbali na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW, 1979) na mapendekezo ya Baraza la Usalama (UNSC 1325 (2000) yanatambua na kutoa haki kwa wanawake kushiriki uchaguzi kama wapiga kura na wanaowania nafasi za uongozi, wanaoteuliwa na kugombea hatimaye kushinda katika nafasi mbalimbali za uongozi kupitia uchaguzi.

Mintarafu ushiriki huu wa wanawake katika siasa na uongozi, Mkurugenzi wa Women Fund Tanzania (WFT), Profesa Ruth Meena, anasema: “Licha ya sheria kuruhusu kuwapo kwa viti maalumu kwa wabunge na madiwani ili kuongeza idadi ya wanawake katika bunge, bado utaratibu wa viti maalumu unawabagua wanawake kwa vile hawapati fursa ya kuteuliwa katika nafasi za juu ikiwamo ya kuwa waziri mkuu.”

Kwa mujibu wa Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania (1977), waziri mkuu huteuliwa na rais miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa kutoka chama cha siasa chenye wabunge wengi.

Anaongeza: “Mfumo huu bado ni kandamizi kwa kuwa wabunge wa viti maalumu hawapewi fedha za jimbo, na kuna nafasi ambazo hawawezi kuteuliwa.”

Aidha, watu mbalimbali wanasema, hakuna mfumo ulio wazi na unaoeleweka wa kuchagua wagombea wa viti maalumu. Wanasema mfumo uliopo si mzuri kwa vile unapenyeza mwanya wa upendeleo, unyanyasaji na ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya viongozi wanaoshiriki uteuzi kwa vile wengine katika vyama kadhaa, huutumia kama mwanya kuwadai wanawake rushwa ikiwamo ya ngono.

Changamoto kama hizo, lugha za kejeli, matusi, ubaguzi na nyinginezo ukiwamo uandishi wa habari unaojikita kwa habari hasi dhidi ya wanawake ukiziacha habari nzuri, ndizo zimelifanya shirika la kimataifa la UN–Women (Tanzania), kukifadhili Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na wadau wengine, kuendesha mradi wa ‘Wanawake Wanaweza’.

Mradi unatoa mafunzo kwa wanahabari mintarafu namna ya kuibua changamoto zinazowakumba wanawake katika harakati za kushiriki siasa na uongozi.

Mradi wa Wanawake Wanaweza, unalenga kuwawezesha wanahabari kujua namna ya kuzibaini, kuzikabili changamoto za ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, kuhamashisha na kuwaelimisha wanawake ili wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ama wa kuchaguliwa, au kuteuliwa katika kada mbalimbali kadiri ya sifa na uwezo wao halisi.

Katika moja ya mafunzo hayo, wanahabari walioshiriki waliazimia kujenga utamaduni wa kuandika na kutangaza habari chanya kuhusu wanawake hata wakati wa kampeni, tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna ‘ugonjwa’ kwa wanahabari wengi kuwaandika wanawake kwa habari ‘hasi’ pekee.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, anawataja wadau wengine katika mradi huo kuwa ni African Women Leaders Network (AWLN), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), na taasisi ya Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF).

Chapisho liitwalo ‘Ilani ya Uchaguzi ya Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi Uchaguzi Mkuu 2015: Agenda ya Mwanamke, Turufu ya Ushindi 2015!’ linasema vyama vya siasa ni mhimili mkubwa wa demokrasia shirikishi na ya ushindani.

Nayo Ibara ya 39 (1)(c) ya Katiba ya Tanzania inasema, kila anayewania uongozi wa kisiasa anapaswa kupendekezwa na chama chake cha siasa, hivyo, ni wazi vyama vya siasa ni walinzi wa lango kuu la kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.

“Hivyo, vyama vina uwezo mkubwa wa kuamua ni nani aingie kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na nani atolewe, vile vile nani ashinde,” linasema chapisho hilo.

Linasema, wanawake ambao ni wapiga kura wakuu, wakatae kuuza haki zao na wakatae kurubuniwa na vyama, viongozi au watu wenye uchu wa madaraka na tabia ya kudhalilisha wapiga kura wao.

“Wakatae kuunga mkono vyama au viongozi watarajiwa wanaokumbatia mfumo dume katika uchaguzi...” Linasema chapisho.

Katika matukio na mazungumzo tofauti, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben, anasema katika uchaguzi mwingine wowote ujao, wanawake wanapaswa kushirikishwa mapema na kikamilifu katika mchakato wote ili wajiamini zaidi huku wakijengewa utayari zaidi kukabili changamoto zinazolenga kuwakatisha tamaa.

Anasema wanawake wana uwezo mkubwa kiuongozi ndio maana wanakwenda shambani huku wengine wakiwa wajawazito, lakini wakati huohuo, wakihudumia familia na mambo yote kwenda vizuri.

Kwa mujibu wa Rose, wanawake waliopata nafasi za uongozi, hawana budi kupanga mikakati madhubuti kuhusu namna ya kuendelea kuwepo na wengine kuongezeka kwa kuonesha wigo mpana wa uongozi, ujasiri, uwezo na kujitokeza kuzungumzia masuala ya wanawake katika vyombo vya habari ambavyo ni fursa yao nzuri kupaza sauti.

Hivi karibuni Tamwa kilikutana na wabunge wanawake jijini Dodoma kujadili kuongeza idadi ya wanawake katika siasa na uongozi ili kufikia 50 kwa 50 katika bunge lijalo mwaka 2025 maana kuisha kwa uchaguzi mmoja, ndiko kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine.

Kwa mujibu wa taarifa, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, alisema: "Ni vyema Tamwa mmekuja mapema katika kipindi hiki cha uongozi cha miaka mitano maana tuna mambo mengi ya kuweka sawa na wanawake wenzetu…”

“Idadi hii ya wabunge inatakiwa kuongezeka; walio katika viti maalumu wajengewe uwezo kwenda kugombea majimboni na wengine waingie viti maalumu.”

Tulia anasema, wanawake wabunge waliochaguliwa na kuteuliwa jukumu lao si tu kuwakilisha vyama bungeni, bali pia kuwatumikia wananchi ili kuongeza idadi ya wanawake viongozi na kufikia 50/50.

Kuhusu umuhimu wa wanawake katika uongozi, mmoja ameandika kwenye ukurasa wa twita: “Nafasi za kiuongozi kwa wanawake ni muhimu katika kuunda mikakati na kuibua suluhisho kwa changamoto zinazowakabili yakiwamo magonjwa ya mlipuko kama Covid-19.”

Watetezi mbalimbali wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanasema umefika wakati mifumo na katiba za vyama zitoe nafasi sawa kwa wanawake na wanaume ili wanawake nao wapate nafasi za kiutendaji.

“Kuna haja Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuviwekea shinikizo vyama vyote kutoa nafasi za uongozi za kiutendaji hata kwa wanawake; tena kwa usawa,” anasema Mhariri wa Habari wa Gazeti la Sauti ya Mara wilayani Tarime, Christopher Gamaina.

Gamaina anasema kwa kuwa nafasi za kiutendaji katika vyama ni hasa uenyekiti na ukatibu mkuu, uwepo utaratibu wa kikatiba katika vyama kuwa, kama mwenyekiti atakuwa mwanaume, basi katibu mkuu awe mwanamke; na kama makamu mwenyekiti atakuwa mwanamke, naibu katibu mkuu awe mwanaume ili kuleta 50/ 50 yenye mantiki.

Chanzo: habarileo.co.tz