Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vitatu kukosa mawakala

D9528acafc5c60e85b43786ba37762db Vyama vitatu kukosa mawakala

Sat, 24 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VYAMA vya siasa vya UMD, UPDP na SAU katika Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza havitakuwa na mawakala watakaoingia katika vituo vya majumuisho ya kura za rais, ubunge na udiwani baada ya kushindwa kuwateua kwa wakati.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilemela, John Wanga, alibainisha hayo katika hafla ya kuwaapisha wagombea ubunge na mawakala wao kutoka vyama saba vya siasa vya CCM, ADC, ACT-Wazalendo, Chadema, DP, Demokrasia Makini na NRA, baada ya kukidhi masharti ya uteuzi kama yalivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wanga alisema taarifa za kuwataka mawakala wa vyama hivyo zilitumwa kwa uongozi wa juu wa vyama vyao ili wawasilishe majina ya mawakala wao kwa mujibu wa sheria, lakini viongozi wao walisema wangeyawasilisha majina ya mawakala wa vyama vyao wao wenyewe.

Alisema hadi jana vyama hivyo vilikuwa bado havijawasilisha majina ya mawakala wao na kufafanua kuwa, muda wa kisheria wa kuyasubiri majina yao hadi jana ulikuwa umekwisha.

"Hii maana yake ni kwamba, kwa sasa hatuna mawakala wa vyama hivyo kwenye jimbo letu la uchaguzi na hatutarajii kumwona wakala yeyote anayetokana na vyama hivyo kwenye vyumba vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura na tukimkuta yeye ni mhalifu," alisema Wanga.

Wanga alisema wagombea ubunge na mawakala hao wa vyama vya siasa waliapa kiapo cha kutunza siri kwa mujibu wa kanuni ya 50(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge ya Mwaka 2020 na kanuni ya 43 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (uchaguzi wa madiwani) za mwaka 2020.

Gazeti hili limewashuhudia mawakala hao wakiapa mbele ya msimamizi huyo wa uchaguzi huku wakitakiwa kutunza siri ya kapo chao ili kuwezesha uchaguzi wa mwaka huu kufanyika kwa huru na haki.

Kwa upande wa kampeni za uchaguzi zilizoanza Agosti 26, mwaka huu na kutarajiwa kuhitimishwa Oktoba 27, mwaka huu, alisema zinaendelea vizuri katika jimbo lake.

Alisema kila mgombea anafanya mikutano yake ya kampeni kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Kamati ya Kuratibu Ratiba ya Kampeni za Ubunge.

Kila chama kinachoshiriki kina mjumbe na vivyo katika ngazi ya kata.

Alisema Jimbo la Ilemela lina vituo vya kupigia kura 795 vilivyotawanyika katika Kata 19 kwa idadi tofauti vikiwa na wapiga kura 302,589 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Kuhusu vifaa vya kupigia kura, alisema tayari NEC imeishapeleka vifaa mbalimbali vya kupigia kura na idadi ya vifaa vilivyopokewa hadi sasa imefikia asilimia 90 ya vifaa vyote vinavyohitajika.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ilemela kwa tiketi ya CCM, Dk Angeline Mabula, alisema kampeni za uchaguzi jimboni humo zinaendelea vizuri na kwamba anaamini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni wa huru na haki.

Chanzo: habarileo.co.tz