Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama sita vyatoa msimamo mzito

32328 Pic+vyama Viongozi wa UKAWA

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unguja. Vyama sita vya upinzani vilivyokutana faragha visiwani Zanzibar kwa siku mbili, vimetoa matamko mazito mawili, huku vikitangaza rasmi kwamba mwaka 2019 ni wa kudai demokrasia.

Uamuzi huo ni historia kwa upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992. Uamuzi mzito wa kwanza ulikuwa Oktoba 2014 pale vyama vinne viliposaini makubaliano saba ya ushirikiano kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Maazimio ya uamuzi huo yaliyosomwa na mwenyeji wa mkutano huo ambaye ni katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni kufanya mikutano ya hadhara inayoruhusiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imezuiwa na wanasiasa wanaoifanya wamefunguliwa kesi mahakamani.

Pia, Maalim Seif alitangaza kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini kupitia chama hicho, Esther Matiko pamoja na wanasiasa wote wa upinzani walioko mahabusu ni wafungwa wa kisiasa na wataitangazia hivyo dunia.

Mbowe na Matiko wako rumande baada ya kufutiwa dhamana kutokana na kuruka dhamana hiyo katika kesi ya jinai inayowakabili kwenye Mahakama ya Kisutu.

“Tunatangaza kuwa sasa ni wakati sahihi na muhimu wa kuongeza umoja, mshikamano na kujitoa kwetu katika kuiendea ajenda yetu ya kitaifa ya kulinda demokrasia,” alisema mwanasiasa huyo aliyekuwa ameongozana na viongozi wengine wa upinzani akiwamo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

“Tutaunda kamati ya kuratibu hatua za kuunganisha makundi ya wananchi nchi nzima na kundi lolote la wananchi, popote walipo, iwe ni wafanyakazi wanaopinga kupunjwa pensheni, wakulima wanaokosa soko la mazao yao, wavuvi wanaonyanyasika, wanafunzi wanaokosa mikopo, wanasiasa wa upinzani wanaokamatwa na polisi bila sababu watafikiwa ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kupigania haki zao,” alisema.

Pia, alisema watapambana kuhakikisha Mbowe na Matiko ambao wako mahabusu pamoja na mahabusu wenzao wa kisiasa nchi nzima wanapewa nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru, mbele ya mahakama na mbele ya macho ya umma.

Tamko hilo lilitiwa saini na Maalim Seif (CUF), James Mbatia (NCCR - Mageuzi), Oscar Makaidi (NLD), Salum Mwalimu (Chadema), Hashim Rungwe (Chaumma) na Zitto Kabwe (ACT - Wazalendo).

Oktoba 2014, vyama vinne vya upinzani viliandika historia mpya baada ya kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano, kubwa likiwa kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi.

Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Hata hivyo, miongoni mwa waanzilishi wa umoja huo; Profesa Ibrahim Lipumba na Dk Wilbrod Slaa walijitoa.

Muungano huo wa Ukawa ulimsimamisha Lowassa kuwania urais katika uchaguzi mkuu 2015.



Chanzo: mwananchi.co.tz