Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama roho kwatu vifaa vya uchaguzi

Fb0ce9c886b718f049ab0314fb72702f Vyama roho kwatu vifaa vya uchaguzi

Sat, 17 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VYAMA vya siasa nchini vimeridhishwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya kusambaza vifaa vya kupigia kura kwa zaidi ya asilimia 80 katika halmashauri mbalimbali nchini.

Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Manunuzi na Usafirishaji ambayo inaundwa na vyama vya siasa, NEC, taasisi za umma na serikali walieleza kuridhishwa na hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo ilikutana jana kwenye Bohari ya NEC Dar es Salaam na kutembelea moja ya maghala ya kutunzia vifaa vya kupigia kura. Pia walishuhudia upakiaji wa vifaa hivyo kwenye magari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Baadhi ya vifaa walivyooneshwa ni pamoja na majalada ya watu wasioona ambayo yana nukta nundu, fomu za matokeo na sehemu ya kupigia kura (kituturu).

Mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Chama cha Demokrasia Makini, Costa Kibonde alisema: “Tumekagua, tumeshuhudia vifaa vipo vingi na vya kutosha na usambazaji unafanyika kwa kasi kubwa.”

Kabendera Eugine wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), alisema ana amani moyoni baada ya NEC kuwaonesha vifaa halisi vya kupigia kura pamoja na kushuhudia kazi ya usambazaji wake.

“Naamini uchaguzi utaenda vizuri,” alisema Eugine. Naye Rodrick Rutembeka wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alishukuru Tume kwa kuwaita na kuwaonesha kazi ya usambazaji wa vifaa ikiendelea vizuri.

Awali, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Asina Omary, alisema lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukagua maendeleo ya usambazaji wa vifaa hivyo.

Katibu wa Kamati hiyo, Emannuel Urembo, alisema ifikapo Oktoba 24 mwaka huu, vifaa vyote vya kupigia kura vitakuwa vimesambazwa kwenye halmashauri zote nchini.

Urembo alisema zaidi ya asilimia 80 ya vifaa vimeshasambazwa kwenye halmashauri mbalimbali.

Chanzo: habarileo.co.tz