Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama 5 vyakemea kampeni za uvunjifu amani

E0e18de3f53fe4f643ffda91b578fde3 Vyama 5 vyakemea kampeni za uvunjifu amani

Sun, 20 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAGOMBEA watano wa nafasi ya urais wanaoviwakilisha vyama mbalimbali, wamekemea lugha za uvunjifu wa amani, zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa katika mikutano mbalimbali ya kampeni inayoendelea nchini.

Waliojitokeza na kuzungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ni Queen Sendiga kutoka Chama Cha Alliance Democratic (ADC), Mutamwenga Mgaywa wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Philipo Fumbo wa Democratic Party (DP), Said Maalim Seif wa Chama cha Wakulima (AAFP) na Cecilia Mwanga wa Chama cha Demokrasia Makini.

Katika mkutano na waandishi, wagombea hao walisema hawaridhishwi na uendeshaji wa kampeni, unaofanywa na baadhi ya vyama na wagombea wao wa nafasi mbalimbali, kutokana na kujaa lugha zinazoashiria umwagaji wa damu, suala walilosema hawakulitarajia katika kampeni zinazoendelea.

"Amani ya taifa hili ni jambo la msingi sana, kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wao kunadi sera zinazochochea uvunjifu wa amani ni kuhatarisha amani tuliyonayo hapa nchini, tukumbuke kuna maisha baada ya uchaguzi " alisema Sendiga

Alitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi( NEC) na vyombo vya ulinzi na usalama, kuongeza umakini kwa kufuatilia wanasiasa wote na vyama vya siasa vinavyotoa kauli hizo. Alisema lugha hizo zimekuwa zikichochea chuki miongoni mwa Watanzania na zisipodhibitiwa mapema, zinaweza kuleta madhara.

Mgombea Urais wa AAFP, Seif, alisema vyama vyote vya siasa ni wamoja na vipo kwa ajili ya kusubiri ridhaa za wananchi, hivyo havipaswi kueneza chuki zozote, kwa kigezo cha kutaka madaraka.

Seif alisema wagombea wote, wanapaswa kutambua kuwa hadi sasa kila aliyepo katika mchakato huo ni mshindi, kwa kuwa uchaguzi haujafanyika, hivyo hawapaswi kueneza chuki kama njia ya kujihami mbele ya wananchi.

Mgombea Urais kwa Demokrasia Makini, Mwanga alisema siasa siyo ugomvi, hivyo hakuna sababu kwa wagombea kueneza lugha za chuki kwa wananchi ili kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Alisema wanachotakiwa kufanya wakati huu ni kuzungumza sera zao kwa wananchi, ili kufanikisha malengo waliyojiwekea, watakapopewa ridhaa na wananchi kuongoza baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba28, mwaka huu.

Kwa upande wao, mgombea wa SAU, Mgaywa na Fumbo wa DP, walisema amani na upendo ndiyo sera ya vyama vyao na tangu kuanza kwa kampeni wamekuwa wakiihubiri, hivyo vyama vingine viige.

Karipio la vyama hivyo kwa vyama vinavyoshutumiwa, kutumia lugha za uvunjifu wa amani ambavyo hata hivyo havikutajwa majina, limekuja zikiwa zimesalia siku 39 kabla ya uchaguzi mkuu unaoshirikisha wagombea urais kutoka vyama vya siasa 17 .

Chanzo: habarileo.co.tz