Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama 14 vyamwangukia Samia kuhusu demokrasia

BAYO Vyama 14 vyamwangukia Samia kuhusu demokrasia

Tue, 25 Oct 2022 Chanzo: Ippmedia

Muungano wa vyama 14 vya upinzani nchini, umemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kupitia haraka na kuifanyia kazi ripoti ya kikosi kazi ili kutatua mambo ya msingi ikiwamo ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa.

Aidha, vyama hivyo vimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kutekeleza maagizo yaliyo chini yake kuhusu ripoti hiyo itakayotolewa na Rais  ikiwamo mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ili viwe na uhuru wa kufanya shughuli zao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa Baraza la Vyama vya Siasa, Doyo Hassan, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa vyama kutokana na ripoti hiyo na kupongeza juhudi za serikali kukamilisha mchakato huo.

“Sisi tunamwomba Mheshimiwa Rais atufanyie haraka kidogo hasa katika masuala ya kanuni na sheria za mikutano ya hadhara na ruzuku za vyama vya siasa ili tuweze kujiendesha na huko mtaani muone kazi zetu na sera zetu kama vyama na vya siasa na tuisaidie nchi.

“Ukisoma mapendekezo manane yaliyotolewa katika muhtasari siku ile, kuna masuala ya mabadiliko ya vyama vya siasa kwa ajili ya kuweka miundombinu mizuri ya siasa na demokrasia nchini. Hili liko chini yake msajili,” alisema.

Doyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) alisema ripoti hiyo imesheheni masuala yote yanayohusu vikwazo vya kisiasa  nchini, hivyo anaamini kama Rais ataifanyia kazi na kuitolea maagizo, itarudisha uhuru wa demokrasia nchini.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema ameshangazwa na kitendo cha baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuipinga ripoti hiyo ilhali hawajui kilichoandikwa ndani kwa kuwa bado haijawekwa hadharani.

“Tulitaraji kuona Watanzania tunajipa muda wa kusoma kwa kina yale yaliyowasilishwa kwa Rais na wajumbe wa kikosi kazi badala ya kukimbilia kupinga yale yaliyosomwa kama sehemu ya muhtasari katika ripoti ile,” alisema Boyo.

Alisema vyama vya siasa vina uhuru wa kutoshiriki kutoa maoni na ni sehemu ya uhuru wa kikatiba lakini kutoshiriki kwao kusionekane kama jambo hilo halifai kwa sababu wako waliokubali kushiriki.

Maoni ya chama hicho ya kukosoa ripoti hiyo na kuwataka wananchi kupinga yale yaliyowasilishwa na kikosi kazi, alisema ni mambo ya kupuuzwa kwa sababu walihusishwa viongozi mbalimbali wa nchi wakiwamo wa dini, wanasiasa na wanazuoni.

“Huwezi ukapuuza maoni na mawazo ya viongozi waliolisukuma taifa letu mpaka hapa tulipo kwa sababu zako binafsi. Tumeona hili jambo si sawa, mawazo ya chama kimoja hayawezi kuharibu jambo liliofanywa na watu wengi kwa kutumia pesa nyingi,” alisema.

Katibu Mkuu wa Democratic Party (DP), Felix Makua, alisema kuundwa kwa kikosi kazi hicho kulitokana na mkwamo wa kisiasa hasa katika upande wa mikutano ya hadhara na katiba. Katika vikao vyao, CHADEMA waligoma kushiriki jambo wanalolitafsiri kama ni ubinafsi.

Muungano huo unaundwa na vyama vya African Democratic Alliance (ADA-TADEA) , ADC, ACT-Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Tanzania Labour (TLP), United Democratic Party (UDP), Demokrasia Makini (MAKINI) na DP.

Vingine ni Civic United Front (CUF), NCCR-Mageuzi, Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National Reconstruction Alliance (NRA).

Ripoti hiyo ilikabidhiwa Oktoba 22, mwaka huu, ikiwa na mapendekezo 18 yaliyogusa maeneo mbalimbali kwa ustawi wa demokrasia nchini.

Chanzo: Ippmedia