Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viziwi wataka NEC kuwafanya wajue kinachoendelea katika uchaguzi

Dca96e80339c61c85a581c99d280b741.png Viziwi wataka NEC kuwafanya wajue kinachoendelea katika uchaguzi

Sun, 23 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), kimeisihi Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kuandaa mazingira rafi ki ya upatikanaji wa habari kwa viziwi zinazohusu masuala ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa CHAVITA TAIFA, Nidrosy Mlawa, alisema suala la upataji wa habari ni haki za binadamu na lipo kisheria.

“Tuiombe Tume ya Uchanguzi kuandaa mazingira rafiki ya upataji wa habari zinazohusu uchaguzi kwa kuweka wakalimani wa lugha ya alama wanapotoa matangazo ili kundi la viziwi nalo liweze kushiriki kikamilifu,” alisema.

Mlawa pia alitoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo havina wakalimani wawaweke ili viziwi nao wanufaike.

“Pia wahariri wapanue au kuongeza ukubwa wa picha ya mkalimani ili aweze kuonekana vizuri kwa macho kwani kwa sasa picha zinazowekwa ni ndogo hivyo kuwafanya viziwi kutumia nguvu sana kuangalia picha wakati wa kufuatilia matangazo,” alisema.

Alisema vyombo vya habari hususani televisheni na kwenye video vinavyowekwa kwenye mitandao navyo vihakikishe vichwa vya habari au maandishi yanayopita yanaendana na tukio linaloonekana kwa wakati huo.

“Tunataka kichwa cha habari kikionesha vijana wa JKT wakimaliza mafunzo basi tuwaone wakipiga kwata, lakini kukiwa na kichwa cha habari hicho na picha inayoonekana ni bustani za mboga inakuwa inatuchanganya sisi kama viziwi na kushindwa kuelewa habari husika,” alisema.

Aidha, Mlawa alitumia fursa hiyo kuwasihi wakalimani kwenda kujisajili Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ili waweze kutambuliwa kisheria na waweze kutoa huduma mbalimbali kwa viziwi nchini.

Ofisa Jinsia wa CHAVITA TAIFA, Lupi Mwaisaka alisema ili viziwi waweze kushiriki ipasavyo kwenye mchakato uchaguzi na kujua sera za vyama ni lazima awepo mkalimani.

Chanzo: habarileo.co.tz