Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita vya sheria mpya ya vyama kuhamia kortini

48111 Pic+sheria

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais amesaini Sheria ya Vyama vya Siasa Februari 13, lakini vita ya kuipinga haijaisha; Chadema imesema itahamishia harakati hizo mahakamani.

Chadema imechukua uamuzi huo baada ya kuona mambo mengi yaliyolalamikiwa na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia, yamo kwenye sheria iliyosainiwa na Rais John Magufuli.

Miongoni mwa mambo waliyolalamikia ni sheria kumpa nguvu kubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama mamlaka ya kutaka taarifa yoyote kutoka chama cha siasa au kiongozi wake au kufuta mafunzo yaliyoandaliwa na chama, udhibiti katika utoaji wa elimu ya uraia na kudhibiti ushirikiano wa vyama.

“Hatuwezi kufurahia hayo marekebisho,” alisema John Mrema, ambaye ni mkurugenzi wa itikadi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema.

“Yote yaliyokuwa yanapingwa na wapinzani yamepitishwa, tunajiandaa kuizuia, japo mahakama zetu ndiyo hizo.”

Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge mwezi Januari, ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa vyama vya siasa na wadau kama wanasheria na wale wa demokrasia wanaohofu kuwa itabana zaidi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini.

Related Content

Baadaye, Mrema alituma taarifa akieleza kuwa sheria hiyo ni mbaya kutokana na vifungu vyake ama kukiuka Katiba au misingi ya utawala bora na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imetia saini.

Lakini, kama ilivyokuwa awali CCM imekubaliana na sheria hiyo ikisema ni safi na wataiheshimu.

CCM yafurahia

Akizungumzia sheria hiyo, Humphrey Polepole ameisifu akisema chama hicho kimejipanga kufuata Katiba na sheria.

“Yako safi kabisa,” alisema Humphrey Polepole, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM.

Hata hivyo, Chadema imesema hawaridhiki na sheria na watakwenda mahakamani kuipinga.

Awali, Mrema alitaja vifungu vinavyoumiza vyama kuwa ni pamoja na kifungu cha 3 (b) kinachompa Msajili jukumu la kusimamia uchaguzi wa ndani wa vyama ikiwa ni pamoja na uteuzi wa wagombea uongozi.

Alisema kifungu cha 3 (g) kinamfanya Msajili kuwa mshauri wa sSerikali kuhusu vyama vya siasa, jambo ambalo alisema linamwondolea sifa ya kuwa mlezi.

Ingekuwaje kwa Maalim Seif?

Pia, kwa mujibu wa Mrema, kifungu cha 8C (2) kinachotaka kila chama kutunza orodha ya wanachama, viongozi wa kila ngazi na jumuiya zake ambayo msajili anaweza kuihitaji wakati wowote. Mrema alisema watashauriana na vyama vingine vya siasa na wadau kuona njia nzuri zaidi ya kufungua shauri mahakamani mapema iwezekanavyo.

Mambo yaliyopitishwa

Wakati wa kupitisha sheria hiyo, hoja kubwa iliyozua mjadala ni ya utoaji wa elimu ya uraia ambayo pia lililalamikiwa na wadau. Katika sheria iliyosainiwa, imeongezwa kifungu cha 5A,B na C.

Kifungu cha 5A(1) kinataka mtu yeyote au taasisi itakayoomba kufanya mafunzo ya uraia au kutoa mikakati ya chama cha siasa, itoe taarifa ya siku 30 kwa Msajili ikieleza aina ya mafunzo, watu watakaohusika, misaada ya mafunzo na matokeo yake.

Kifungu cha 5A(2) kinasema Msajili anaweza kufuta mafunzo au mpango wa kuwajengea uwezo, akitoa sababu ya kufanya hivyo. Kifungu kidogo cha 3 kinatoa adhabu kwa mtu atakayekiuka sheria hiyo kulipa faini ya si chini ya Sh500,000 na isiyozidi Sh5 milioni au kwenda jela miezi mitatu au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote.

Pia kifungu kidogo cha 4 kinasema adhabu kwa taasisi itakayokiuka sheria hiyo kuwa ni faini isiyopungua Sh5 milioni na isiyozidi Sh30 milioni.

Mbali na adhabu hizo, mtu au taasisi itakayokiuka kifungu hicho itatakiwa impelekee Msajili taarifa za mafunzo hayo kwa kipindi husika na ikishindwa kifungu cha 6 kinasema itakuwa imefanya kosa.

Kuhusu vikundi vya ulinzi, marekebisho hayo yamepiga marufuku, na sheria inataka ulinzi ufanywe na Jeshi la Polisi au taasisi yoyote ya ulinzi ya Serikali, pia inapiga marufuku mafunzo yenye mfumo wa kijeshi yenye kuhusisha nguvu au matumizi ya aina yoyote ya silaha.

Kwa mujibu wa kifungu kidogo cha 3, chama kitakachokiuka kifungu hicho kitafutwa na kwa kiongozi au mwanachama atakayekiuka atashtakiwa na adhabu yake ni kifungo cha kuanzia miaka mitano jela lakini kisizidi miaka 20 au vyote kifungo na faini.

Sharti vyama kushirikiana

Sheria hiyo pia inaruhusu ushirikiano wa vyama kabla na baada ya uchaguzi, lakini vifungu vya 11A na 11B vinaweka masharti ya kumtaarifu Msajili kuhusu makubaliano hayo ambayo pia yanatakiwa yapitishwe na mikutano mikuu.

Kifungu kidogo cha 3 kinasema makubaliano yatakayofanywa na vyama kabla ya uchaguzi, yanatakiwa kufanyika miezi mitatu kabla ya uchaguzi huo na kwa yale yatakayofanyika baada ya uchaguzi yanatakiwa kumfikia Msajili siku 14 baada ya kupitishwa.

Kifungu kilichokuwa kinazungumzia uwezekano wa vyama kuungana na kuwa kimoja kwa malengo maalumu, hakikupita.

Kifungu kingine ambacho kilipigiwa kelele na kimepitishwa kwenye marekebisho, ni cha 21E kinachompa mamlaka Msajili kumsimamisha mwanachama yeyote wa chama kufanya kazi za siasa.

Kifungu kidogo cha 2 kinakataza vyama vinavyoshiriki uchaguzi au shughuli ya kisiasa kikishirikisha mtu aliyefungiwa kufanya siasa.



Chanzo: mwananchi.co.tz