Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita mpya kati ya Dk Bashiru na Membe

29760 Membe+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukombe/Dar. CCM imeingia katika vita mpya dhidi ya wagombea urais wa mwaka 2015, baada ya katibu wake mkuu, Dk Bashiru Ally kumtuhumu hadharani Bernard Membe kuwa anakwamisha mikakati ya urais 2020.

Awali CCM ilipambana vikali na Edward Lowassa, aliyejivua uanachama mwaka 2015 na ikawavua uanachama watu waliosemekana kuwa walikuwa wakikisaliti chama kwa kumuunga mkono waziri huyo mkuu wa zamani wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Jana, Dk Bashiru alirudia wito wake kwa Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wa kumtaka aende ofisini kwake wakati akiwa mkoani Geita. Alikuwa akijibu ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya mtandaoni na mtu mwenye jina la Bernard Membe.

Vita hiyo ndani ya CCM, inatokea kipindi ambacho umebaki takriban mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Membe, aliyekuwa mbunge wa Mtama, alikuwa miongoni mwa makada 38 waliojitosa kuwania kupitishwa na CCM kugombea urais. Hata hivyo, aliishia katika tano bora.

Wengine katika tano bora ni January Makamba, Amina Salum Ali, Asha-Rose Migiro na Dk John Magufuli, ambaye alipitishwa na kushinda urais.

Tangu 2015, Membe amekuwa hajihusishi na masuala ya kisiasa na mara chache huonekana kwenye matukio ya kijamii.

Sehemu pekee aliyojitokeza hadharani kuzungumzia siasa ni wakati alipofanya mahojiano na Mwananchi na kukosoa uendeshaji wa Serikali mwanzoni mwa 2016.

Lakini sakata aliloanzisha Dk Bashiru linaanzisha vita mpya dhidi ya mtaalamu huyo wa diplomasia.

Juzi, Dk Bashiru akiwa mkoani Geita alisema Membe anatuhumiwa kuandaa mipango ya kumkwamisha Magufuli katika uchaguzi wa Rais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana naye.

“Kati ya wagombea wote (wa urais mwaka 2015) wa CCM ni Membe pekee yake ambaye sijakutana naye. Namkaribisha ofisini, aje anieleze ninayoyasikia ni kweli au si kweli,” alisema Dk Bashiru katika mkutano huo.

“Kwani haya yanayozungumzwa nyie hamyasikii? Nasema peke yangu? Mimi ndiyo katibu mkuu wa CCM, aje ajitetee kwamba yeye si kikwazo.

“Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020, kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu.

“Sasa mimi nakualika uje ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya uanachama wa CCM ya kusema kweli daima fitina kwangu mwiko. Njoo ofisini ueleze.”

Baada ya wito huo, kulisambaa ujumbe katika mitandao ya kijamii ulioandikwa na mtu aliyejiita Bernard Membe.

“Kufuatia taarifa za kwenye mitandao jioni (juzi) hii na jumbe nyingi zinazotumwa kwangu kwa wingi, nimeamua kutoa ujumbe huu kwa wote wanaonitakia mema,” anasema mtu huyo.

“Usiku huu nimempelekea katibu mkuu wa chama chetu, ndugu Bashiru ujumbe wa kukubali kumuona mara nitakaporejea kutoka nje ya nchi

“Nimeshangazwa kidogo na utaratibu uliotumika kuniita, lakini kwa sababu ya ugeni kazini na kwa sababu ninamheshimu, nitakwenda kumuona ofisini kwake.”

Katika ujumbe huo, ‘Membe’ huyo anasema siku atakayokwenda ofisini kwa Dk Bashiru, mtu anayemtuhumu kuandaa mkakati wa kumng’oa Rais Magufuli, naye awepo ili kuthibitisha tuhuma hizo.

Hata hivyo, Dk Bashiru alikataa sharti hilo akisema huo si utaratibu wa CCM kukutana na wanachama wake.

“Sikumsema Membe kama mtu maarufu au mwenye nguvu, bali kama mwanachama wa kawaida. Hana tofauti kabisa na wanachama walioingia leo, ila ana tofauti kwa kuwa amekuwa waziri na mbunge,” alisema Dk Bashiru.



Chanzo: mwananchi.co.tz