Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vipindi vigumu alivyopitia mbunge Kabati

33492 Pic+kabati Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kati ya vipindi vigumu alivyowahi kupitia Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati ni pale majina ya wabunge hao yalipotangazwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, na lake kuwa halipo.

Lakini kati ya vipindi vya furaha kwake ni miezi mitatu baadaye, jina lake lilipotangazwa kuwa naye ni miongoni mwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabati ambaye anawakilisha makundi yote ya wanawake wa mkoa wa Iringa bungeni anasema, kinachoweza kurejesha heshima mahali popote alipo mwanamke ni kazi zake na kusimamia haki.

“Nalimshukuru Mungu jina langu lilipotangazwa, siku zote huwa naamini nyuma yangu wapo watu wananiombea hasa ninao watumikia,” anasema.

Katika ziara yake kwenye ofisi za Mwananchi, Kabati aliongozana Anitha Daniel (14) mtoto mwenye ulemavu ambaye alikuwa miongoni mwa walemavu 25 aliowaleta jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwachongea viungo bandia.

Kabati anasema anawasaidia walemavu hao akiamini siasa ni pamoja na kuona wale wanaokuzunguka wanafurahia maisha kwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi na kuingiza kipato.

Anasema tangu akiwa mdogo alitamani kuwa mwanasiasa kwa sababu aliamini kuwa hiyo ni nafasi pekee anayoweza kuitumia katika kuwatumikia wananchi.

Anasema alianza siasa kwa kuwania nafasi za chini kama uenyekiti wa mtaa, udiwani na sasa ni mbunge.

Ajira kwa wasichana

Sababu ya wasichana wengi hususani wa Mkoa wa Iringa kukimbilia jijini Dar es Salaam mara baada ya kuhitimu elimu ya Msingi ni Ugumu wa maisha.

Wengi huamini, kufanya kazi za ndani mijini wataweza kupata ahueni ya maisha.

Kabati anasema vilio vya wasichana walioumizwa baada ya kukimbilia mijini kufanya kazi hizo vilimfanya aanzishe kampuni ya usafi, ili wachache waajiriwe na kupewa maarifa.

Anasema mpaka sasa zaidi ya wasichana 40 wamepata ajira katika kampuni hiyo.

Alianzaje siasa?

Kabati anasema, aliamini akiwa mbunge au diwani ndio anaweza kutimiza ndoto zake za kuwa karibu na jamii.

Anasema alianza kuwa mwenyekiti wa tawi, baadaye akawa Diwani viti maalum, jimbo la Ukonga, katika Manispaa ya Ilala na hapo ndipo alipoanza kutimiza ndoto zake.

“Harakati zangu za ukombozi kwa vijana na wanawake nilianza nikiwa Diwani wa Kitunda, manispaa ya Ilala. Cha kwanza ilikuwa ni kufungua kampuni ya Usafi ambayo niliamini nisingehitaji wasomi kufanya nao kazi,” anasema Kabati.

Anasema alianza kwa kutembea vijiweni ili aweze kukutana na vijana hasa wale waliokuwa wakijihusisha na dawa za kulevya.

Elimu

Kabati anasema kiuhalisia hakuna maendeleo yanayoweza kutokea kwenye nchi yoyote kama elimu inasahauliwa.

Anasema kila mdau wakiwamo viongozi wanao wajibu wa kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuinua elimu.

Anasema tangu alipoingia madarakani mwaka 2015 amefanikiwa kutoa kompyuta 20 kwa ajili ya ofisi za walimu wa kuu katika shule za msingi a manispaa ya Iringa.

Anasema mkakati wake ni kuendelea kutafuta wadau wengine kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule kwa sababu nyingi zina majengo yaliyochoka.

Ujasiriamali

Kabati anasema amewekeza zaidi katika kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali wanawake wenzake ili wakipata mitaji waweze kusimamia biashara zao.

Anasema zaidi amekuwa akikutana na wanawake hao kupitia vikundi vya kiuchumi.

“Kwa hiyo kazi yangu ni kuhakikisha kuwa wanapata asilimia 10 zilizogawanywa kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu kukuza mitaji yao,” anasisitiza.

Kabati amefanikiwa kujenga kituo cha Polisi katika eneo la Septemba, manispaa ya Iringa kutokana na uhaba wa vituo hivyo mkoani Iringa.

Mbali na hilo ameshakutana na makundi yote ambayo anaamini anaweza kufanya nayo kazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz