Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini watoa kauli kilio cha tume huru

96991 Tume+hurur+pic Viongozi wa dini watoa kauli kilio cha tume huru

Wed, 26 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Ombi la viongozi wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe la kuwataka viongozi wa dini kuombea uchaguzi mkuu wa 2020, limeitikiwa vizuri na viongozi ambao wanataka haki itamalaki kwa kupatikana tume huru.

Juzi wakiwa katika mazishi ya Mzee Elias Mwingira, ambaye ni baba mzazi wa Josephta Mwingira, mtume wa Kanisa la Efatha, viongozi wa kisiasa walitumia msiba huo kuwa fursa ya kudai kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Pia viongozi hao walimuomba Mtume Mwingira, kushirikiana na viongozi wengine wa madhehebu mbalimbali kuliombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba.

Wanasiasa, hasa wa upinzani, wanasema tume ya sasa ya uchaguzi, NEC, haiko huru kutokana na muundo wake hasa viongozi na watendaji wake kuteuliwa na Rais-- na walishinda katika kesi ya kupinga wakurugenzi wa wilaya kuwa wasimamizi, lakini Serikali ikakata rufaa na kushinda.

Suala hilo pia lilikuwepo katika Rasimu ya Katiba mwaka 2014, lakini mchakato ukakwama katika hatua ya kura ya maoni.

Pia Soma

Advertisement
Hayo yamesababisha viongozi wa kisiasa, hasa wa upinzani kuendelea na kilio hicho huku wakitaka makundi mengine yaunganishe nguvu, wito wa hivi karibuni ukitolewa na Mbowe katika mazishi juzi.

Viongozi wa dini watahadharisha

Baada ya wito huo, baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, walionekana kuunga mkono wito huo, ila wakatofautiana kuhusu kipi kiwe kipaumbele kati ya kuandika Katiba mpya na tume huru.

“Wanaopaswa kuombewa ni viongozi wote wa Serikali ambao taifa liliomba na kuwapata mwaka 2015,” alisema Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT)alipozungumza na Mwananchi.

“Tulimuomba Mungu (2015) atupe viongozi, akatupa hawa. Ni hawa wanaotakiwa kuombewa.

“Kuomba bila kufanya kazi ni sawa na ushirikina. Ni sawa na kusema amani, haki, tume huru vije kama muujiza wa kukanyaga mafuta ya upako.

“Mungu tunayemuomba hajatunyima haki, amani wala uchaguzi huru na wa haki.”

Lakini Askofu mstaafu wa Jimbo la Kilimanjaro la Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Glorious Shoo, alionya kuwa kama haki inapokosekana mahali popote duniani, inaweza kuondoa amani ya taifa.

“Kwa kawaida hata kama haki ipo na inatolewa, lakini kuna haja kwa wanaoitoa kujiridhisha wao na kuwaridhisha wanaoipokea, waone kweli ipo,” alisema Shoo ambaye alisema maoni hayo ni yake na si ya kanisa.

“Mahali popote haki ikahisiwa tu, inaweza kuondoa amani na kwa sababu hiyo kuna haja kwa wote wanaohusika na utoaji haki watafute kila njia ili kuonyesha haki inatendeka.”

Hata hivyo, Askofu Alinikisa Cheyo wa Jimbo la Kusini Magharibi la Kanisa la Moravian, alivishauri vyama vya upinzani kujikita zaidi kudai mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1977.

Askofu Cheyo alisema suala la upinzani kuanza kudai tume huru ya uchaguzi ni sawa na kufumua mfumo wa Katiba kuanzia hewani badala ya kuanzia katika msingi wenyewe kwa kudai mabadiliko ya Katiba.

“Labda wangekuwa wanazungumzia zaidi kuhusu Katiba. Kwa sababu hufumui mfumo kwa kuanzia hewani tu, unaanzia pale katika msingi. Na sheria mama ni katiba,” alisema Askofu Cheyo.

“Mimi nadhani wangejikita zaidi kuzungumzia mabadiliko ya Katiba tuliyonayo sasa, halafu ndio wazungumzie tume huru ya uchaguzi.”

Alisema anaamini kati ya Watanzania milioni 50, ambao wako katika vyama hawazidi milioni 10 na hata yeye hana kadi ya chama chochote na sehemu kubwa ya wachungaji wake ni hivyo hivyo.

Kwa upande wake Alhad Mussa Salum, sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, aliunga mkono wazo la kuwepo kwa tume huru, akisema hiyo itasaidia kuivusha nchi.

“Kuwepo kwa tume huru ni jambo jema kwa sababu uchaguzi pia utakuwa huru. Tunaunga mkono mchakato huu wa kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi,” alisema Sheikh Alhad.

Vilevile, katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda alisema suala la tume huru ya uchaguzi haliwezi kuepukika kwa mazingira ya sasa endapo kunahitajika uchaguzi huru na haki utakaoleta viongozi bora.

Chanzo: mwananchi.co.tz