Unguja. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kusini Unguja, kimewataka viongozi na watendaji wake ngazi ya matawi na majimbo kufanya ziara za mara kwa mara kwenye taasisi za Serikali ili kubaini changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Mei 30, 2019 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo, Abdulaziz Hamad Ibrahim katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, katika vituo vya afya kwenye Jimbo la Paje Unguja.
Alisema endapo viongozi wa ngazi hizo wataendeleza utamaduni wa kufanya ziara hizo, itasaidia kupunguza changamoto zilizopo kwenye sekta mbalimbali za utoaji huduma kwa wananchi.
Alisema kupitia ziara hiyo ya siku mbili kwenye vituo vya afya vya majimbo ya Makunduchi na Paje, imesaidia kubaini changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma za afya.
Alisema CCM inatekeleza Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020 kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha wananchi wa mijini na vijijini wanapata huduma kwa viwango vinavyostahili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, maofisa utabibu wa vituo hivyo vya afya, waliipongeza Serikali Kuu kwa kufanya ugatuzi ambao umeongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi hususan wa vijijini.
Pia Soma
- Wizara ya Sheria na Katiba yasema ndoa kwa wahanga wa udhalilishaji husababisha kesi za udhalilishaji kutomalizika
- Shahidi mgonjwa akwamisha kesi
- Kiongozi mbio za mwenge awaasa wahandisi