Viongozi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kichama wa Selous (Wenye Majimbo ya Tunduru Kusini, Tunduru Kaskazini na Namtumbo) waliokuwa na kesi ya kushambulia na kujeruhi katika Mahakama ya Wilaya Tunduru wameachiwa huru baada ya kukutwa hawana kesi ya kujibu.
Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu wa ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande amewataja viongozi hao kuwa ni Mtutura Abdallah (Katibu wa mkoa), Said Njinga (Kiongozi wa ACT Amani Mkoa), Yasin Mawila (Mwenyekiti Jimbo la Tunduru Kaskazini) na Issa Thabit (Mwanachama).
Amesema kuwa viongozi hao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka Mei 13 mwaka jana kwa tuhuma za kuwashambulia na kuwajeruhi Wanachama wa CCM waliovamia eneo lililopaswa kufanya Mkutano wa ACT na kutaka kufanya Mkutano wa CCM wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Ligoma Jimbo la Tunduru Kusini Mwezi Mei 2021.
"Chama cha ACT Wazalendo kinawapongeza Mawakili walioisimamia kesi hiyo na kuhakikisha kuwa haki inapatikana.Tunamshukuru Wakili wa kujitegemea Prosper Kaizelege na Wakili wa Chama, Victor Kweka ambaye alisimamia kesi mwanzoni.
Tunatoa wito kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kuacha kutumika kisiasa wakati wa Uchaguzi kwa kuwakandamiza wapinzani na kukibeba chama tawala. Jeshi la Polisi litekeleze majukumu yake kwa weledi na kuzingatia Sheria.," amesema Maharagande