Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi Halmashauri Kuu CCM kukutana jumamosi hii Lumumba 

A488e781cd2fff04be6d734497ece656 Viongozi Halmashauri Kuu CCM kukutana jumamosi hii Lumumba 

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Philip Mangula na Ali Mohammed Shein kutoka Zanzibar watakutana Jumamosi hii katika Kikao Cha Halmashauri Kuu katika ofisi za chama hicho zilizopo Lumumba Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho mkoani Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM), Humphrey Polepole amesema kikao hicho kitafanyika saa 8:00 kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali.

Akielezea namna chama hicho kilivyopokea taarifa za kifo cha Rais Magufuli, Polepole amesema kuwa “Chama cha Mapinduzi na safu yake ya uongozi kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Dk John Magufuli.

Aidha amefafanua kuwa chama hicho kitakuwa kwenye maombolezo ya siku 21 sambamba na tangazo la Serikali na kwamba wakati wote huo bendera za Chama Cha Mapinduzi zitapepea nusu mlingoti.

Rais Magufuli, alifariki dunia jana jioni akiwa na umri wa miaka 61, baada ya kuugua kwa muda mfupi kutokana na maradhi ya moyo aliyokuwa akisumbuliwa nayo kwa zaidi ya miaka 10.

Kifo cha Rais kilidhibitishwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye alihutubia Taifa na kusema kuwa Rais Magufuli, alifariki majira ya saa 12 jioni jana katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Chanzo: www.habarileo.co.tz