Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala, anadaiwa kumtwanga mangumi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) katika mkoa huo, Ramadhani Shabani.
Hali hiyo ilitokea juzi Septemba 20, 2022 saa nane mchana katika ukumbi wa RRC Sumbawanga, ambapo kikao cha kujadili majina ya wagombea nafasi ndani ya chama hicho kilifanyika.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, chanzo cha kutwangana ngumi kati ya viongozi hao wa chama hicho tawala ni kupishana kauli baada ya kukatwa jina la mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenezi Wilaya ya Sumbawanga vijijini.
“Chanzo kilikuwa ni kushutumiana kupokea rushwa na kurushiana maneno, ndiyo mwenyekiti wa mkoa akatoka jukwaa kuu na kumfuata huyo wa UVCCM wakaendelea kubishana na baadaye huyo wa mkoa akamtandaka miguuni huyo wa UVCC,” kilisema chanzo hicho.
Alisema kwa desturi ya chama hicho, nafasi za uongozi huombwa kuanzia chini na kujadiliwa na vikao mbalimbali kabla ya uchaguzi wenyewe.
Alisema katika tukio hilo, kikao kilikuwa kinajadili nafasi ya uenezi wa chama hicho Wilaya ya Sumbawanga vijijini, awali Sekretarieti ya chama hicho ndani ya wilaya hiyo ilipitisha majina matatu kugombea nafasi hiyo na yalivyofika kwenye Kamati ya Siasa wilaya, jina moja likakatwa.
Alisema Sekretarieti ya Mkoa ilivyokaa, ilirudisha jina lililokatwa na mchakato ukaendelea kwenye Kamati ya siasa ya Mkoa ambayo ilipitisha majina kama yalivyoletwa na sekretarieti ya Mkoa.
Alisema Halmashauri Kuu ya mkoa ilipokaa, jana chini ya, Lukala ambaye ndiye pia alikuwa kiongozi kwenye kamati ya siasa mkoa, alionekana kutaka kuyageuka maamuzi yake ya awali.
“Hapo sasa ndipo shida ilipoanzia, watu wakawa wanahoji kwanini mwenyekiti anataka kula matapishi yake, ni kitu gani kimetokea,” alisema.
Alisema baada ya hali hiyo, shutma za kupeana rushwa zilizidi, ambapo upande mmoja ulikuwa unadai wanaotaka jina lisikatwe wamekula rushwa na upande mwingine unasema wanaotaka kukata jina wamekula rushwa za Sh 50,000.
Alisema katika hali hiyo, mwenyekiti wa UVCCM alisimama na kuhoji kwanini wajumbe waliopitisha majina kwenye Halmashauri ya Mkoa sasa wanataka kupindua maamuzi yao wenyewe.
Katika hali isiyo ya kawaida, inadawa mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa alishuka jukwaani na kumfuata mwenzake wa UVCCM na kuendeleza mabishano ambapo mwishoni alimrushia Makonde.
Hali hiyo ilifanya kikao hicho kuvunjika kwa muda na kurejea baadaye baada ya usuluhishi kufanywa.
“Tulivyorudi ndani, mwenyekiti wa mkoa alitaka huyo wa UVCCM atoke nje, yule kijana aligoma akisema yeye ni mjumbe halali wa hicho kikao na hawezi kutoka labda apewe barua rasmi,” kiliendelea kupasha chanzo chetu.
Baada ya mzozo huo, Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliamua Kamati ya Siasa Mkoa yote ipelekwe kwenye kamati ya maadili wachunguzwe juu ya tuhuma za rushwa walizotoleana.