Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi 80 Chadema kupiga kambi Hai

15821 Viongozi+pic TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitawatumia viongozi wake 80, kufanya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata mbili za Jimbo la Hai.

Bado haijawekwa wazi endapo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, ataongeza nguvu ya kampeni kunyakua kata hizo.

Uchaguzi katika kata hizo unafanyika baada ya waliokuwa madiwani wake, Yohana Laizer wa Kia na Robson Kimaro wa kata ya Machame Uroki kwa tiketi ya Chadema, kujiuzulu na kujiunga na CCM.

CCM kimewateua Laizer na Kimaro kupeperusha bendera yake wakati Chadema kimemteua Albashiri Kombe kugombea kata ya Machame Uroki na Hassan Kibuo, kuwania kata ya Kia.

Akizungumza na gazeti hili leo Septemba 5, Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema timu hiyo ya viongozi 80, itahusisha wabunge wawili wa chama hicho wa mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Lema, wabunge hao watakaopiga kambi katika jimbo hilo ni Mbunge wa Rombo na mwenyekiti wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Joseph Selasini na wa viti maalum, Grace Kiwelu.

“Ni kweli hadi sasa hatujaonyesha kashikashi yoyote lakini nataka nikuhakikishie tumejipanga na leo (jana) tunakwenda Hai na kikosi kikubwa cha wapambanaji,”alisema Lema.

Mbali na wabunge, lakini Lema alisema kikosi hicho kitashirikisha madiwani 67 kutoka kata za Moshi Manispaa (24), Moshi Vijijini (19), Hai (20) na kutoka Jimbo la Siha watakuwemo madiwani wanne.

Lema alifafanua kuwa mbali na wabunge na madiwani, lakini timu hiyo itahusisha viongozi wa Chadema wa ngazi ya mkoa na wilaya, ambao watasambaa katika vitongoji vya kata hizo.

Alipoulizwa kama Mbowe ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo atashiriki kampeni hizo, Lema alikataa kuweka wazi ujio wake, akisema huenda kiongozi huyo akafika katika mikutano ya lala salama.

Kwa upande wake, katibu wa CCM Kilimanjaro, Jonathan Mabhia, alisema chama chake kwa sasa kinaendelea na mikutano ya ndani na kampeni za nyumba kwa nyumba katika kata hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz