Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana watakiwa kuhoji mabadiliko sheria ya vyama vya siasa

31686 Vijanapic Upinzani Tanzania

Sat, 15 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wa mabaraza ya vijana ya vyama vya upinzani nchini wamewataka vijana kuendeleza mjadala wa kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Mabaraza sita ya vijana ya vyama hivyo yamekutana leo jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kupinga muswada huo unaopingwa na uongozi wa juu wa vyama vyao.

Akisoma tamko la viongozi wa mabaraza hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema wameupitia muswada huo na kubaini unalenga kukwamisha ushiriki wa vijana katika siasa za Tanzania.

“Vijana wote nchini popote mlipo tuendeleze mjadala huu kwa sababu hili ni jambo linatugusa wote. Tuendelee kuelimishana na kuupinga kwa nguvu muswada huu ambao haulitakii mema Taifa letu," alisema Sosopi.

Alidai vyama vinatoa mafunzo mbalimbali kwa vijana ili kuwajengea uwezo lakini muswada huo ukipitishwa fursa hiyo itakuwa ni ridhaa ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ambaye anaweza kuzuia au kukubali kufanyika kwa mafunzo hayo.

Sosopi alisema kifungu cha 21(e) cha muswada huo kinampa mamlaka msajili kumvua uanachama mtu yoyote katika chama cha siasa na kudai jambo hilo linaweza kusababisha vijana wenye nguvu na ushawishi kwenye siasa kufukuzwa uanachama.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), Hamidu Bobali alisema anashangazwa na kitendo cha msajili wa vyama vya siasa kujiwekea kinga kwenye muswada huo, huku akidai hatua hiyo ni kujihami kwa yale anayopanga kuyafanya.

"Msajili ana wasiwasi gani mpaka awekewe kinga kwenye muswada huo, kwamba hawezi kushtakiwa kwa uamuzi wowote atakaoutoa. Hilo linatupa wasiwasi kwamba wamejipanga kuua upinzani nchini," alisema.

Mabaraza yaliyokutana ni Bavicha, Juvicuf, Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, kitengo cha vijana cha NCCR Mageuzi, jumuiya za vijana za UPDP na Chaumma.



Chanzo: mwananchi.co.tz