Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana waonywa kutumika kwenye maandamano

Cce99c60d86da7127898048cd7d1903e Vijana waonywa kutumika kwenye maandamano

Thu, 22 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZIKIWA zimebakia siku sita kabla ya Watanzania kupiga kura vijana wameonywa kukataa vishawishi vya kuandamana ili kufanya ghasia siku ya uchaguzi.

Huku vijana nao wakitakiwa kujiepusha na vishawishi vya kuandamana, ikiwa ni pamoja na kutumiwa kufanya ghasia kwamba huo ni uvunjifu wa amani na watakabiliwa na sheria za nchi.

Rai hiyo ilitolewa na wajumbe wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Rukwa katika tamko lao la pamoja walilolitoa jana mjini hapa baada ya kumalizika kwa kikao chao cha ndani kisha wakakutana na wanahabari.

Akisoma tamko hilo kwa wanahabari mjini Sumbawanga, Kaimu Katibu wa Kamati hiyo, Mchungaji Adam Sikazwe alisema viongozi wa dini wakiwa wadau wa amani mkoani Rukwa kwa pamoja wanatamka kwamba kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu kwamba kuna baadhi ya watu wanaojitokeza kuwachochea vurugu ili kusababisha uvunjifu wa amani ndani ya nchi kupitia kauli na matendo yao.

Akifafanua alisema kwa upande wa viongozi wa dini imebainika baadhi yao pia wanajihusisha na watu wanaohamasisha vijana kufanya fujo na kuandamana kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

“Sisi viongozi wa dini ambao ni wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Rukwa tunawaomba viongozi wote wa dini wasijihusishe kabisa na watu hao wanaowahangaisha vijana kufanya ghasia kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 28,” alisema Mchungaji Shikazwe ambaye pia ni Katibu Mkuu Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Sumbawanga.

Tamko hilo linasisitiza kuwa kazi kubwa ya taasisi za dini ni kuhubiri amani na umoja wa raia nchini kwa kuwa ni tunu Watanzania waliozawadiwa na Mwenyezi Mungu.

Pia wamewataka watu na taasisi zote ambazo ni wadau wa amani kuzingatia kutenda haki, misingi ya sheria kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi huo.

Pia kuheshimu taratibu ziliwekwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani na utulivu.

Awali, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo alisisitiza viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha amani nchini inaendelea kudumishwa wakati huu na baada ya uchaguzi ili shughuli za kijamii na kiuchumi ziendelee kwa usalama kwa ustawi wa nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz