Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana kutopiga kura sababu zatajwa

Nusrat Hanje Mbunge Mbunge wa Viti Maalum, Nusrat Hanje

Tue, 21 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Viti Maalum, Nusrat Hanje amesema tatizo la kiuchumi kwa vijana ni kikwazo kwa kundi hilo kushiriki kwenye uchaguzi.

Aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipozungumzia mdahalo wa vijana utakaofanyika Mei 25, 2024 unaolenga kuzungumzia miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, Hanje.

Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, mkutano huo utakwenda kuweka viwango vya aina ya vijana wanaohitajika Tanzania.

Mbunge huyo alisema kuwa katika mdahalo huo watajadili ushiriki wa vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Alisema ni vyema vijana wakawania nafasi kuanzia katika serikali za mitaa na vijiji hadi ngazi za kitaifa. Vyama vya siasa vina jukumu la kuweka vijana chini ya miaka 35 kwenye uteuzi wa wagombea.

"Lakini kuna changamoto za kiuchumi kwa vijana chini ya miaka 35, hasa katika wabunge wanaume. Wao hawana nafasi ya viti maalum, ni lazima ukagombee, kijana gani anaweza kuwa na uwezo wa kiuchumi kwenda kuchangia?" Alisema.

Nusrat alisema hata kuendesha kampeni kunahitaji fedha, lakini kijana ndio kwanza ametoka chuoni, "anajitafuta kiuchumi" ili kupata fedha za vipaza sauti na magari ya kufanya kampeni.

Alisema taifa linahitaji vijana ambao wanaweza kujenga hoja, wanaoweza kushauri, siyo kusifia tu viongozi. Hata Rais Samia Suluhu Hassan alishasema "serikali ikosolewe kwa hoja.

Mbunge huyo alisema ni matumaini yake kuwa baada ya mkutano huo watakuwa na vijana wanaoweza kujenga taifa na si wabeba mikoba ya viongozi au "chawa" ambao hawashauri panapohitajika.

"Isionekane kama ni 'uchawa' mtu akiamua kuzungumzia vizuri kiongozi wake kama amefanya vitu vizuri. Mahali ambapo unatakiwa kushauri bado unasifia, wakati mwingine labda mwenyewe amekwama anatakiwa kushauriwa, lakini wewe unasifia. Tutajadili hilo," alisema.

Mbunge huyo alisema mdahalo huo utahusisha makundi ya vijana kutoka jumuiya ya vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali za elimu.

Alisema wawakilishi wa wizara zinazojishughulisha na masuala ya vijana watashiriki pia katika mdahalo huo pamoja na viongozi wa vijana kwenye vyama vya siasa vya CCM, ACT-Wazalendo, CUF na vingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live