Dar es Salaam. Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limemuomba Rais wa Tanzania, John Magufuli kuzungumzia sintofahamu kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Limesema ukimya wake kuhusu uchaguzi huo unaogusa wananchi wengi utakaofanyika Novemba 24, 2019 unatia shaka.
Vyama saba vya siasa; Chadema, ACT-Wazalendo, NLD,CUF,UPDP, Chauma na NCCR-Mageuzi vimejitoa katika uchaguzi huo kwa madai ya kutotendewa haki ikiwa ni pamoja na wagombea wake kuenguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 14, 2019 mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi kunyamazia dhuluma wanazofanyiwa wananchi kunaashiria anafahamu kinachoendelea.
“Hatumlazimishi ila ajue kwamba Watanzania wamedhulumiwa haki zao hivyo azungumzie mustakabali wa uchaguzi huu,” amesema Sosopi.
Baraza hilo limemtaka pia Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kujiuzulu kwa madai ya kuuvuruga uchaguzi huo unaosimamiwa na wizara hiyo. Sosopi amedai Jafo ametoa kauli zinazoashiria ilipangwa uwe uchaguzi wa chama kimoja.
“Jafo anapaswa kujua kuwa ameshindwa kusimamia uchaguzi ajiuzulu na kama atashindwa kufanya hivyo, Bavicha tutamtaka rais amfute kazi,” amesema Sosopi.