Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo 2,000 kuwania nafasi 30 NEC-CCM

Ccm Pic Wafuasi wa CCM wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Kivumbi kinatarajiwa kutimka ndani ya CCM kutokana na mchuano mkali wa makada zaidi 2,000 wa Bara na Zanzibar, walioomba kuwania nafasi 30 za kapu za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Miongoni mwa waombaji hao, wale watakaoteuliwa na NEC kesho, watapigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa chama hicho keshokutwa.

Mkutano mkuu huo utakaofanyikia kwa siku mbili katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, unatanguliwa na vikao vya kamati kuu leo na NEC kesho, vyote vikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.

Mbali na wajumbe hao wa NEC, mkutano huo utawachagua viongozi wa juu wa chama hicho, mwenyekiti wa makamu wake wawili -- Bara na Zanzibar na kuhitimisha uchaguzi ya ndani ya chama.

Kwa Zanzibar, CCM itampata makamu mwenyekiti mpya Zanzibar baada ya Dk Ali Mohamed Shein kumaliza muda wake na nafasi hiyo kulingana na utamaduni wa chama hicho, itachukuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Wakati nafasi hizo za juu hazina mvutano kutokana na utaratibu wake kufahamika na wanaoziwania kuwa wagombea pekee, mvutano unasalia katika nafasi hizo za wajumbe wa NEC ambazo pia hutoa picha ya nguvu za kisiasa alizonazo mhusika ndani ya chama.

Wagombea wanaotajwa kuwa miongoni mwa hao 2,000 wakiwania nafasi 30 (15 bara na 15 Zanzibar), ni Sophia Simba, Waziri wa Nishati, Januari Makamba pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Wengine wanaotajwa ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Saadala ‘Mabodi’ na Waziri wa Ulinzi na JKT, Innocent Bashungwa.

Pia wamo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, Katibu wa NEC, siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu idadi hiyo, Shaka alisema ni namba kubwa ambayohaijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

“Hii inaonyesha demokrasia ndani ya chama imesimika mizizi, wanachama wana imani kuwa usawa na haki vitasimamiwa kikamilifu ndani ya chama,” alisema Shaka.

Shaka alisema katiba ya CCM hivi sasa imetoa nafasi 30 za wajumbe wa NEC, 15 wakitoka Tanzania Bara na 15 Zanzibar.

“Hata hivyo, kwa sababu bado vikao vinaendelea nafasi hizi zinaweza kuongezwa, lakini kwa katiba yetu ya sasa ni nafasi 30 zinazogombewa,” alisema.

Taarifa za ndani zilieleza nafasi hizo zinaweza kuongezwa kutoka 15 hadi 20 kwa pande zote za Bara na Zanzibar na kufikia wajumbe 40 badala ya 30.

Akifafanua zaidi kuhusu wingi wa wagombea, Shaka alisema hiyo inaonyesha mwamko na matokeo ya mwenyekiti kukitengeneza upya chama hicho hadi kuwa na nguvu kubwa nchini.

Alisema hali hiyo inajionyesha hata viongozi wa Serikali wanapofanya ziara katika maeneo mbalimbali huripoti katika ofisi za chama na pia kushusha chama chini.

Akizungumzia wingi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Lufunyo Hussein alisema katika muktadha wa demokrasia au utawala bora hali hiyo inaweza kuchukuliwa kama hatua ya kuheshimu misingi ya utawala bora.

“Kwa maana mmeweka taratibu na mnaziishi kwa hiyo kitendo cha kuwa na chaguzi za mara kwa mara ni ukomavu wa utamaduni wa kichama na utamaduni wa kuheshimu kanuni na taratibu walizojiwekea wao wenyewe,” alisema.

Akieleza matarajio yake, Dk Shadidu Ndossa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, alisema matumaini yake mkutano huo utatumika katika kuwapata viongozi wazuri na wenye maono.

“Wapatikane viongozi watakaoisimamia Serikali, hasa mawaziri wanaomsaidia Rais Samia kama ilivyo ni kuwa wabunge, mawaziri, ma RC (wakuu wa mikoa) na DC (wakuu wa wilaya) wote ni wawakilishi wa chama. Sasa kama CCM itapata viongozi wazuri watasaidia sana kusimamia ilani,” alisema.

Maandalizi ya mkutano

Katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma tayari pamepambwa na bendera za CCM na mabango na Shaka alisema maandalizi ya mkutano huo yanaendela vizuri.

Huu ni mkutano wa pili kwa Rais Samia tangu aingie madarakani na tangu achaguliwe kushika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho Aprili 30 mwaka jana.

Rais Samia, mwenyekiti wa sita wa CCM, alipitishwa kushika wadhifa huo kwa kura 1,862 sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa na wajumbe wote katika mkutano huo.

Ushindi wa Rais Samia, uliambatana na kupanga upya safu ya uongozi katika chama hicho, ikiwa ni pamoja na kuwateua makada mbalimbali kuwa viongozi wa juu wa chama hicho kinachounda Serikali.

Viongozi hao ni pamoja na Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu Daniel Chongolo na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.

Katika mkutano wajumbe wengi wanatarajiwa kuwa wapya baada ya kuwa wapya baada ya wengi wao kuangushwa katika chaguzi za ngazi za wilaya, mkoa na jumuiya za chama hicho.

Mkutano huo pia utakuwa na kazi ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli zilizofanywa na Serikali kwa muda wa miaka mitano ambazo zitawasilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Hali ya kibiashara

Hata hivyo tofauti na mikutano iliyopita ambapo CCM ilikuwa ikiwashikia nafasi wajumbe wake na hivyo wageni wengine kukosa nafasi, nyumba nyingi za kulala wageni zina nafasi katika siku zote mbili za mikutano hiyo.

Naye Mkazi wa Airport, Ashura Hamis alisema wanasubiri ugeni huo kwa kuwa vyakula watapika katika mkutano huo vitawawezesha kupata kipato.

“Mimi nimekuwa nikipata nafasi ya kuuza chakula katika mikutano, tunawasubiri wajumbe waje tuuze chakula, vinywaji na nyama choma maana ndiyo msimu wa kuuza sana,” alisema.

Chanzo: Mwananchi