Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amesema hadi kufikia jana Jumatatu Oktoba 14 saa 12 jioni, Watanzania milioni 15.54 sawa na asilimia 68 walijiandikisha katika Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24,2019.
Katika tathimini, Jafo amesema mkoa wa Dar es Salaam, umeingia kwenye orodha ya mikoa sita inayofanya vizuri kwa kushika nafasi ya pili huku Kilimanjaro ikiendelea kubaki kwenye mikoa inayosuasua, ikifuatiwa Kigoma na Arusha hadi.
Jafo ametoa kauli leo Jumanne Oktoba 15, 2019 wakati akitoa tathimini ya uandikishaji katika mikoa mbalimbali nchini, akisema hivi sasa kumekuwa na mwitikio tofauti na mchakato ulivyoanza.
"Malengo ya Tamisemi ni kuandikisha wapiga kura wapatao 22, 916, 413 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Tangu tulivyoanza mchakato huu mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Lindi na Iringa ndiyo ilifanya vizuri hadi jana jioni," amesema Jafo.
Amefafanua mkoa wa Pwani ndio unaongoza kwa kuandikisha Watanzania 473, 639 sawa na asilimia 80, ukifuatiwa na Dar es Salaam, 2, 064, 820 (77%), Tanga 823,194 (76%), Mtwara 530,523 (75%), Lindi 353,649 (75%) na Iringa 381,134(74%).
Jafo amesema hadi sasa mkoa wa Kilimanjaro umeandikisha wapiga kura 444, 954(48%), Kigoma 555, 856 (53%) na Arusha 551,614 (59%) akisema yote ipo chini katika mchakato huo.
Pia Soma
Mbali na hilo, Jafo amewaonya Watanzania watakaobanika kujiandikisha mara mbili akisema ni miongoni mwa makosa makubwa na adhabu ya ni faini Sh300,000 au kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.Waziri huyo ametumia nafasi hiyo, kuvishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uandikishaji wa daftari la wapiga kura, akisema vimefanya kazi nzuri.
Vitambulisho vinavyokubaliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa hivi hapa
Uandikishaji huo ulioanza Oktoba 8, utamalizika Oktoba 17, 2019.
Waziri Jafo: Uchaguzi serikali za mitaa Novemba 24
Waziri Jafo awaita Dodoma Ma RC, RAS kuhusu uchaguzi serikali za mitaa