Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wanaoshusha bendera za CUF, kupandisha za ACT waonywa

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unguja. Wakati harakati ya ushushaji na upandishaji wa bendera na kubadilisha rangi matawi ya CUF  kuwa ya ACT- Wazalendo zikiendelea maeneo mbalimbali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja visiwani Zanzibar limesema halitasita kuchukua hatua za kisheria harakati hizo zikiendeshwa kinyume na sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Thobias Sedoyeka amebainisha hayo leo Jumanne Machi 19, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwembe Madema Mjini Unguja.

Amesema licha ya shughuli hiyo kuendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali, lakini alitahadharisha kwa wafuasi hao watekeleze shughuli zao hizo kwa kufuata sheria za nchi pamoja na utaratibu na kanuni za uendeshaji wa vyama vya siasa.

“Tunasikia kuna watu wanatia rangi matawi yao pamoja na kushusha (bendera za CUF) na kupandisha bendera za ACT- Wazalendo, tunachowaomba sisi wafanye shughuli zao hizo kwa kufuata sheria.”

“Ila kama itatokezea kuna ishara ya kufanyika uvunjifu wa amani hatutasita kuchukua hatua stahiki mara moja,” amesema.

Kamanda Sedoyeka amesema si jambo la busara hata kidogo kuona hivi sasa amani ya nchi inaendelea kuwa katika hali nzuri kisha wakajitokeza watu wachache wakaichafua kwa maslahi yao au kisingizio cha siasa.

Ametoa wito kwa wafuasi na wananchi mbalimbali wanaoshiriki shughuli hizo kuendelea kutunza amani huku akisema Jeshi la Polisi limejipanga vyema kiulinzi katika maeneo yote.

Soma zaidi: Zitto amkabidhi Maalim Seif kadi namba 1, Babu Duni namba 10



Chanzo: mwananchi.co.tz