Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wana CCM watofautiana Membe kufukuzwa uanachama

Video Archive
Mon, 2 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kumfukuza uanachama Bernard Membe umepokewa kwa hisia tofauti na wanachama wa kawaida wa chama hicho tawala.

Wakati wengine wakisema uamuzi huo ni sahihi kulingana na taratibu za chama hicho, baadhi wamesema angeweza kuonywa tu kama ilivyokuwa mwaka 2014 ambapo alituhumiwa kuanza kampeni mapema pamoja na wenzake watano huku suala la mgogoro ndani ya CCM na mtego wa kisiasa kwa wapinzani vikitajwa.

Peter John mkazi wa Arusha alisema hafahamu sababu iliyotajwa kama ni kweli, “walisema alifanya makosa hayo hayo mwaka 2014 ambayo chama kilimchukulia hatua za kinidhamu.”

Mwanachama mwingine wa CCM Arusha, Zephania Mollel alisema kumfukuza inaonesha jinsi chama hicho kinavyokabiliwa na mgogoro wa ndani ambao unaweza kuathiri hata utendaji kazi wa Serikali.

“Sababu iliyochangia kufukuzwa ni msimamo wake usiyoyumba wa kutoa maoni namna anavyoona nchi inaongozwa. Mfano suala la kubana matumizi, Membe alikosoa hiyo hatua hadharani baada ya hapo amekuwa anachukuliwa kama adui,” alisema Mollel

Naye Yoeza Mnzava mkazi wa Dodoma alisema Membe alikuwa mwanachama wa muda mrefu lakini pale mtu anapoonekana anakosea sheria lazima zichukuliwe dhidi yake.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“CCM ina kanuni, taratibu na sheria zake, hakuna aliyeko juu yake pale mtu anapoonekana anaenda kinyume lazima awajibishwe,” alisema Mnzava.

Pia Innocent Chuwa alisema ni jambo la kawaida kwa chama chochote cha siasa kuwawajibisha wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuwahoji wanachama kwa kuwa kinaendeshwa kwa kanuni na taratibu zilizowekwa.

Mkazi wa Dar es Salaam, Enock Nyongole alisema chama hicho kimeonyesha ukomavu kumuwajibisha Membe bila kujali walio nyuma yake.

Alisema kilichofanyika kwa Membe na viongozi wengine wa zamani wa CCM kitatoa fundisho kwa wengine waliowahi kudhani nafasi zao zinaweza kuwa kinga ya kufumbia makosa yao.

“Binafsi namshauri Membe atulie tu na kama bado anaipenda CCM aombe msamaha,” alisema.Nyongole.

Olivia Tindwa, mkazi wa Tabata alisema CCM ingetoa onyo kwa wanachama wote kulingana na makosa yao badala ya kumfukuza mmoja wao.

“Sawa amewajibishwa kulingana na katiba lakini kulikuwa na nafasi ya kumuonywa, angejirekebisha tu,” alisema Tindwa.

Hata hivyo alisema bado kuna wanachama wengine wanaokiuka katiba ya chama hicho ngazi za chini ambao wanapaswa kuonywa na hata kuchukuliwa hatua kama ilivyotokea kwa waliowahi kuwa viongozi wa juu.

Mkazi wa Vwawa-Mbozi mkoani Songwe, Musa Mwangeni alisema CCM imechukua hatua stahili na pia kimewatendea haki ya kuwapa nafasi ya kujitetea.

Matrida Lukas alisema CCM ni taasisi ambapo kila mtu anapaswa kuwa na nidhamu na kufuata kanuni na sheria zilizopo ili kuheshimu kanuni zilizopo.

Mkazi wa Jijini Mbeya, Suleiman Mwambipile alisema pamoja na kuonesha kwamba Membe ametenda makosa yake tangu mwaka 2014, lakini kitendo cha CCM kumfukuza uanachama hivi sasa inaweza kuwa ni mtego wao kwa upinzani.

“CCM Ina mbinu nyingi sana, sitashangaa Membe kuona ametumwa na kwa njia ya kufukuzwa ili ahamie chama moja wapo cha upinzani na akapewa mkoba wa kupeperusha bendera ya kiti cha urais uchaguzi ujao, halafu atafanya kila linalowezekana hatashinda na CCM ikaibuka kidedea tena.” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz