Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Walichozungumza Maalim Seif, Mbatia na Lipumba baada ya kukutana na Magufuli

Video Archive
Wed, 4 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanasiasa wakongwe watatu wa vyama vya upinzani Tanzania akiwemo Maalim Seif, Profesa Ibrahimu Lipumba na James Mbatia wamekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, Ikulu ya Dar es Salaam ambapo baada ya mazungumzo hayo wameeleza kufurahishwa na mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.

Baada ya mazungumzo hayo, Maalim Seif ambaye Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo amesema yeye na Rais Magufuli wamezungumzia masuala ya kudumisha amani, usalama na upendo kwa watu wote, huku akieleza kufurahishwa kwake na dhamira ya Rais Magufuli kukutana na viongozi mbalimbali na kujadiliana mambo yenye maslahi na nchi.

Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amempongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki ambapo pia amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi ya Serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za Taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi.

Lipumba ametoa wito kwa Watanzania wote kuweka uzalendo mbele, kudumisha amani na utawala bora na amewataka wanachama wote wa CUF kujiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Kwa upande wake Mbatia amewataka wanasiasa kuacha  kukamiana na kuchochea mambo hasi dhidi ya Taifa na badala yake waungane kuendeleza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ikiwemo kuboresha elimu, upatikanaji wa nishati na mengine yenye maslahi mapana kwa wananchi.

Mbatia ametoa wito kwa wanasiasa na Watanzania wote kwa ujumla kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya kukumbatia mambo yenye maslahi binafsi na ameipongeza Serikali kwa kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali.

Pia Soma

Advertisement

Chanzo: mwananchi.co.tz