Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Waitara aeleza alivyokuwa ‘jembe’ Chadema

Video Archive
Thu, 16 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara amejisifu kuwa alikuwa ‘jembe’ ndani ya Chadema kwa kuwa ameshiriki kwenye chaguzi ndogo nyingi na harakati za chama hicho.

Akizungumza jana kwenye mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za Mwananchi, Tabata Relini jijini Dar es Salaam, alisema ndani ya Chadema kabla hajahamia CCM, alishirikishwa kuongoza kampeni katika chaguzi ndogo nyingi huku akitoa mfano wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Waitara alisema katika jimbo hilo aliyekuwa mbunge wake, Rostam Aziz (CCM) alikuwa akipita bila kupingwa kwa kuwa upinzani haukuwa na nguvu kwenye eneo hilo.

Alisema wakati wa uchaguzi mdogo baada ya Rostam kujiuzulu, alitumwa na Chadema kumuuza mgombea wao ambapo aliweka kambi kwa miezi minne na kufanikisha mgombea huyo kupata kura nyingi japokuwa hakushinda.

Mwanasiasa huyo alisema kutokana na umuhimu wake ndani ya Chadema kwenye harakati nyingi hasa Operesheni Sangara na mikakati mingine ya maandamano, mara zote alikuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu.

Akizungumzia kutogombea ubunge Tarime, alisema viongozi wa chama hicho akiwamo aliyekuwa katibu mkuu, Dk Wilbroad Slaa walimuomba akagombee Ukonga.

Alisema aliheshimu mawazo ya viongozi hao na kwa kutumia umaarufu wake eneo la Ukonga aligombea na kushinda, huku akisisitiza kuwa hakupata msaada wa kifedha kutoka kwa viongozi wa Chadema.

Waitara alisema siku alipotangaza kujiondoa katika chama hicho, alirudi nyumbani kwa amani kwa kuwa wananchi wake wanampenda.

Kuhusu alichofanya alipokuwa mbunge wa Ukonga, Waitara aliyejiunga na CCM, Julai 28, alisema kwa zaidi ya miaka miwili amefanya mambo mengi.

“Ukonga tumejenga shule nyingi za msingi mpya. Kata ya Mzinga kuna shule mpya, kuna shule Msongola, kata ya Zingiziwa, Buyuni tumejenga zahanati pale Msongola mtaa wa Luhanga, sasa hivi tunajenga zahanati mtaa wa Zinga ya ghorofa na kituo cha polisi,” alisema.

“Kata ya Kitunda kuna mradi wa maji mtaa wa Kipelo, Msongola kuna mradi wa maji umekamilika, tumejenga barabara kutoka Zingiziwa mpaka Chanika tumetumia Sh600 milioni.”

Hata hivyo, alisema alipokuwa Chadema alikuwa akikosa ushirikiano wa wakuu wa wilaya na mkuu wa mkoa ambao ndio wasimamizi wa shughuli za Serikali.

“Sasa fedha yote hii inasimamiwa na Serikali, kwa maana kwamba wakusanyaji wote ni Serikali. Halmashauri inachofanya ni kutenga bajeti. DC (mkuu wa wilaya) ni msimamizi wa shughuli zote za halmashauri akihakikisha kuwa sheria, kanuni na miongozo inafuatwa,” alisema.

“Mkuu wa mkoa ana wajibu wa kuhakikisha kuwa kama kuna kodi zimekusanywa, lazima taratibu zifuatwe.”

Alisema alikuwa akipata vikwazo vya ushirikiano kutoka kwa wakuu hao kwa vile alikuwa mpinzani.

“Ili kikao kiende vizuri ni lazima kuwe na ushirikiano kati ya mwenyekiti na wajumbe wa kikao. Sasa maagizo ya chama, kwa mfano Dar es Salaam, tumeagizwa tushirikiane na mkuu wa mkoa, wakati miradi mingi pale jimboni imekuja kuzinduliwa na Mwenge.”

“Msimamo wa Chadema hawaungi mkono Mwenge, wakisema uwekwe makumbusho. Unatakiwa ufanye jambo lolote kuhakikisha kuwa Chadema iko pale. Sasa hii ni tofauti ambayo tunakosa ushirikiano.”

Licha ya kutaka ushirikiano na wakuu wa mikoa na wilaya, Waitara alisema viongozi wa CCM hawapaswi kukubaliana na wapinzani kwa kuwa kuna ushindani.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akijibu swali la usawa katika ushindani ilhali wakurugenzi wa halmashauri ni wateule wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

“Hizi ni timu mbili tofauti, hapa kuna Simba na Yanga. Huwezi kumpa mbinu mwenzako ya kufunga mechi ili wewe ushuke daraja.

“Mimi siwezi kumsemea Rais, lakini siasa ya nchi hii, siasa ya Afrika na dunia ndivyo ilivyo. Siasa haiko sawa, vinginevyo tungeshinda uchaguzi (wapinzani). Lazima katika ushindani kuna atakayeshinda na atakayeshindwa. Siasa duniani haiwezi kuwa sawa,” alisema.

Aliwataka wapinzani kutosingizia kauli mbalimbali za Rais Magufuli, bali wapambane kwa kuwa kauli hizo ni za kisiasa.

“Kauli za kisiasa zinajibiwa kisiasa, kama Simba akikwambia leo nitakufunga mabao 10 halafu unaacha kwenda uwanjani, uache kucheza mchezo?” alihoji.

Kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, alisema umesaidia kuimarisha demokrasia na uhuru wa mawazo mbadala na umeibua viongozi wapya ambao wasingeweza kuonekana chini ya chama kimoja.

Waitara alisema mfumo huo ni muhimu na asingependa ufe kwa kuwa umemsaidia hata Rais kukusanya baadhi ya hoja za upinzani bungeni na kuziingiza katika ilani ya CCM ambayo anaitekeleza.

Hata hivyo, alisema upinzani katika kipindi hiki unatakiwa kuacha kulalamika, badala yake ujikite katika kuibua changamoto na ajenda mpya zitakazofanyiwa kazi na Serikali.

“Vyama vya upinzani vimetoa fursa ya watu kupata upana wa kufanya siasa, yaani kwa mfano wakati wa chama kimoja wangebanana humohumo (kwenye chama kimoja). Kwa hiyo, kwa sababu ya ufinyu wa nafasi watu wengi wangekosa fursa,” alisema Waitara.

Alisema vyama vya upinzani vimetoa nafasi ya kujadili masuala mengine ambayo yanaendelea kujadiliwa kwa uwazi, akitoa mfano wa hali ya demokrasia nchini.

“Kuna mambo ambayo yanazungumzwa (wakati huu) huenda katika mfumo wa chama kimoja yasingeweza kuzungumzwa. Yako mengi hata hiyo demokrasia tunayoizungumzia ina maana kuna mambo ambayo watu wasingepata nafasi ya kusema ila sasa wanasema.”

Alitaja faida nyingine kuwa ni kupatikana kwa wabunge wenye mawazo mbadala, akisema huenda kuna wanasiasa wasingekuwa wabunge nchi hii kwa sababu ya ufinyu wa nafasi hizo.

“Siyo kila linalofanywa na upinzani ni baya sana, hapana. Yako mabaya ya upinzani na yako mazuri.”

Akifafanua umuhimu wa upinzani, alisema Rais Magufuli alikuwa bungeni kwa miaka 20 na akiwa mbunge aliyesikiliza hoja za wapinzani na bajeti kivuli, ndiyo maana alipoingia madarakani hoja nyingine ameanza kuzitekeleza chini ya ilani ya CCM.

Alipotakiwa kueleza ni kwa nini asingeendelea kubaki upinzani ili kuisukuma Serikali iendelee kuwajibika zaidi kwa wananchi, alijibu: “Huwezi kufanya kazi ya kuibua tu, mimi nimekuja kuongeza nguvu kwa mambo niliyokuwa naamini yanafanyiwa kazi. Niliyaibua, naamini wako wengine wataibua mengine na yataendelea kufanyiwa kazi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz