Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Vyama vya siasa vyataka sheria zibadilishwe

Video Archive
Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vyama vya siasa vimeonyesha wasiwasi kuhusu uchaguzi wa madiwani utakaofanyika mwakani na mkuu wa 2020 kutokana na mazingira ya chaguzi za sasa yalivyo, hivyo kutaka mabadiliko kadhaa ikiwamo ya sheria.

Wakizungumza jana katika mkutano uliovikutanisha vyama vya siasa na Baraza la Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama hivyo walisema yale yaliyoonekana katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, yanadhihirisha kuwa chaguzi zijazo hazitakuwa huru na haki hivyo jitihada zifanyike ili kurekebisha kasoro hizo.

Akitaja maazimio ya vyama hivyo, naibu katibu mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema vimependekeza kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi itakayoundwa na watu wasiofungamana na chama chochote.

“Kwa kuangalia hali inavyojitokeza sasa katika chaguzi ndogo za marudio, kuna kila dalili uchaguzi wa mwakani na ule mkuu kukumbwa na mtafaruku,” alisema Mnyika.

“Kingine ni vyama vya siasa viungane kwenye uchaguzi na kumsimamisha mgombea mmoja na vinapouungana viwe na fursa ya kunadi sera moja. Hata ikiwezekana viruhusiwe kujiua na kuunda chama kimoja vikitaka bila kulazimishwa,” alisema na kuongeza kuwa pia wameshauri mamlaka ya uteuzi isiwe mikononi mwa Rais.

Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba alisema bila kuwapo kwa marebisho katika sheria za uchaguzi, uchaguzi ujao utaliweka taifa katika wakati mgumu.

“Marekebisho ya mpito yafanyike sasa kabla ya kufanyika uchaguzi ujao maana kile tunachokiona kwenye chaguzi hizi za marudio zinazoendelea siyo ishara njema kwa taifa letu,” alisema.

“Tunahitaji kuwa na marekebisho ya sheria maana sasa kumeibuka mbinu mpya za kuwaengua wagombea na hii tukiacha iendelee itatuletea matatizo mbele safari,” aliongeza.

Naibu katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa alisema kama mchakato wa kupata Katiba Mpya umekwama na Serikali ya Awamu ya Tano imeweka bayana kuwa hicho sio kipaumbele chake, kuna haja ya kufanyika marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ili uchaguzi ujao usiwe na kasoro yoyote.

“Wasomi wameshindwa kabisa kujitokeza kujadili masuala ya nchi, Katiba imesusiwa na kuachiwa wanasiasa pekee yao, hakuna cha NGO (mashirika yasiyo ya kiserikali) wala nini hakuna wanaozungumzia kuhusu Katiba, sasa nchi mnaipeleka wapi?” alihoji Mtemelwa.

Renatus Muhabi, Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK) aliwaponda wanasiasa wenzake kwa kutokuwa na umoja na badala yake kuzungukana na kujali zaidi nafsi zao.

Hata hivyo, aliwataka kutovunjika moyo katika juhudi zao za kupigania haki na ikiwezekana akapendekeza kufanyika migomo mbalimbali kama ilivyo kwa baadhi ya nchi nyingine.

Akihitimisha mjadala huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda mbali ya kupongeza utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, aliwataka wanasiasa hao kulitumia baraza hilo kuzitafutia majibu changamoto zinazowakabili.

“Tumieni baraza hili katika kutatua changamoto zenu, kama hujapeleka kesi kwa mkweo hawezi kutoa ufumbuzi wa mgogoro,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz