Dar es Salaam. Kikao cha Baraza la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania cha kujadili tuhuma zinazomkabili Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita kimesimama kwa muda baada ya jina la mjumbe wa Chama cha Wananchi (CUF) kusainiwa wakati hayupo ukumbini.
Kikao hicho kinafanyikia ukumbi wa Karimejee jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Januari 9, 2020 ambacho kabla ya kusimama kilikuwa kikiongozwa na Meya Mwita.
Tukio limesababisha mvutano mkubwa miongoni wa wajumbe wa Chadema na CCM kutaka kushikana mashati wakitakana kupigana.
Mbali na hilo, katika meza kuu hali haikuwa shwari kati ya Naibu Meya, Abdallah Mtinika na Meya Mwita kugombea kipaza sauti wakitaka kuongea ili kutoa ufafanuzi.
Baada ya wajumbe wa Chadema kuingia, Meya wa Ubungo anayetokana na Chadema, Boniface Jacob kushika daftari la mahudhurio na kuhoji uwepo wa jina Kassim Mshamu diwani wa Minazi Mirefu.
"Naomba kutoa taarifa katika hili daftari kuna mjumbe hayupo anaitwa Mshamu ameisaniwa namba 18, lakini mbona hayupo. Mkurugenzi na wewe unasimamia sheria lakini hii sio sawa mmeghushi.”
"Dunia nzima leo inaona mlichokifanya hatuwezi kukubali uhuni mlioufanya leo," amesema Jacob huku akiwaonyesha wajumbe daftari la mahudhurio.
Hatua hiyo ilisababisha mvutano kuzidi kushika kasi hatua iliyosababisha polisi kuingia ndani ya ukumbi ili kutuliza vurugu kati ya wajumbe wa CCM na Chadema.
Polisi baada ya kuingia ndani, wamewatoa ndani ya ukumbi Meya Jacob, Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Asanga kwa sababu hawajasaini daftari la mahudhurio ikiwa ni amri aliyoitoa Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana baada ya kuibuka mvutano wa kutokusaini daftari la mahudhurio.
Meya Jacob amesema hawawezi kusaini daftari ambalo lina makosa ya kughushiwa kwa kuwepo kwa saini ya mjumbe ambaye hayupo.
Lengo la kikao hicho cha madiwani ni kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mwita baada ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuchunguza tuhuma ambazo zinamkabili.
Miongoni mwa tuhuma anazokabiliana nazo Mwita ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.
Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubun-go Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.
Hata hivyo, Mwita alipofika mbele ya kamati hiyo alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo bali ni za kutengenezwa ili kuondolewa katika kiti hicho alichokitumikia kwa miaka minne.