Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema CCM kilipata shida kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutokana na chuki na tamaa za baadhi ya viongozi wake waliowaengua wagombea wenye sifa, kuwaweka wasiokubalika.
Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2020 jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala nchini Tanzania.
Amesema CCM kilijipiga fimbo katika uchaguzi uliopita kutokana na chuki za viongozi na wanachama wake jambo alilodai lilikifanya chama hicho kushindwa katika baadhi ya maeneo.
Amewataka kuwa wamoja katika uchaguzi wa mwaka 2020 ili waweze kushinda maeneo mengi zaidi na kuendelea kuongoza Serikali.
Amesisitiza kuwa chama hicho kina hazina ya watu wengi wenye uwezo wa uongozi na kutaka wapewe nafasi wakijitokeza.
Habari zinazohusiana na hii
- CCM yatenga Sh1 milioni kumchukulia fomu Rais John Magufuli
- VIDEO: Makamu wa Rais Mama Samia aongoza maadhimisho miaka 43 ya kuzaliwa CCM
- Samia awaonya wanachama CCM
Kiongozi huyo ametoa onyo pia kwa wanachama wa walioanza kujipitisha majimboni kwa lengo la kuwania ubunge katika uchaguzi huo.
Amesisitiza anayefaa kugombea apewe nafasi ili kukipa chama ushindi badala ya wanachama hao kuenguliwa au kuvuliwa uanachama ili mradi wasipate nafasi kwa sababu tayari viongozi wana watu wao mfukoni.
“Mtu anafaa kugombea lakini anaandikiwa sifa mbovu, kisha anaenguliwa. Mwenendo huu hautupeleki kuzuri, tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu tushikamane ili twende pamoja, tushinde pamoja,” amesema Samia.