Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema figisu za wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndanda zilimkimbiza Mbunge wa jimbo kupitia Chadema Cecil Mwambe na kuamua kugombea ubunge kupitia chama pinzani.
Rais ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 15, 2019 aliposimama katika jimbo la Ndanda wakati wa ziara yake akienda wilaya ya Ruangwa.
“Mbunge wenu huyu alikuwa mgombea wa CCM alikuwa anakubalika, lakini kwa sababu ya figisu za watu wa huku ndani ya CCM nataka nieleze ukweli mimi huwa napasu aga tu wakaacha kumpitisha akaamua kuhamia CCM kwa hiyo huyu ni wetu mlifanya makosa ninyi wenyewe na mnafahamu makosa ya kukosea kuchagua,” amesema.
Amesema Mwambe alitakiwa awe mbunge wa CCM, hivyo aliamua kumuita Mwambe ili azungumzia suala hilo.
“Niligombea kupitia CCM 2015 niliongoza kura za maoni kwa kuwa nilikuwa sifahamu mfumo mzuri wa chama kipindi hicho kura zangu alipewa mtu mwingine kwa kuwa niliambiwa kura zangu hazikutosha.”
“Lakini Mungu alichagua niwe kiongozi wa Ndanda nilikwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo na nikashinda na ninaahidi nitaendelea kushirikiana na wananchi wa hapa,” amesema Mwambe.
Habari zinazohusiana na hii
Rais Magufuli amesema, “Wakati mwingine tunajicheleweshea maendeleo sisi wenyewe mtu anapenda na wananchi, anakipenda chama lakini figisu za chama mnamnyima mtu anayetaka kushiriki hili liwe fundisho kwa wanachama na wananchi wa huku.”“Mimi niligombea na watu 42 wa CCM ila kiukweli mimi nilikuwa nakubalika hawakunifanyia mzaha wakanipitisha. Wanaokubalika msiwafanyie figisu hiki ni chama chetu sote.”
“Nimekusikia hata ninapokuona moyo wako umejaa CCM ninakuamini na kama upo tayari kuhamia CCM uhamie msimkate tena na ninahitaji watu watakaonipa ushauri mzuri kwa kuwa tunaongea lugha moja inayofanana kama ilivyo kwa Nape,” amesema Rais Magufuli