Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Prof Lipumba apata pigo la kwanza CUF

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imempa pigo la kwanza Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba baada ya kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya chama hicho.

Mahakama hiyo imetengua uteuzi wa wajumbe hao waliopendekezwa na kambi ya Profesa Lipumba na kusajiliwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Wajumbe hao waliteuliwa na Profesa Lipumba kuwa wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kwa madai kuwa wajumbe wa awali wamemaliza muda wao.

Katika uamuzi uliotolewa jana na Jaji Benhajj Masoud alibatilisha uteuzi huo akisema amejiridhisha ulifanyika bila kuzingatia sheria ya Muungano wa wadhamini, ambao ndiyo unasimamia usajili wa wajumbe wa bodi za wadhamini wa taasisi mbalimbali nchini.

Pia, Dk Masoud alisema hata wanachama wa chama hicho waliopendekezwa na kambi nyingine ya chama hicho inayoongozwa na katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad pia hawakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi kwani nao hakuwa wamekidhi matakwa ya sheria.

Hata hivyo, wajumbe wa kambi ya Maalim hawakuwa wanatambuliwa na Rita.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, CUF imekuwa katika mgogoro uliokigawa chama hicho pande mbili ya Profesa Lipumba na Maalim Seif na mgawanyiko huo umefika mpaka kwa wanachama, wabunge, madiwani na viongozi wengine.

Jana, kabla ya Jaji Masoud kuutoa uamuzi huo, vijana wa CUF waliimarisha ulinzi katika ofisi za makao makuu Mtendeni mjini Unguja, Zanzibar.

Mwananchi lilifika katika ofisi hizo na kushuhudia makundi ya walinzi wa chama hicho wakiwa katika hali ya utayari kuhakikisha hakuna anayeingia kama ingetokea kambi ya Maalim Seif inayotumia ofisi hiyo ingeshindwa.

Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama hicho, Omar Shehe akizungumza na Mwananchi juu ya ulinzi huo alisema CUF ina mgogoro katika pande mbili hivyo anaamini lolote linaweza kutokea na ndiyo maana waliamua kuweka ulinzi kupitia vijana wao

Wakati huo, Shehe aliwataka wananchi wasishituke na hali hiyo huku wakisubiri maamuzi ya Mahakama na kile ambacho viongozi wa chama chao watakieleza baada ya vikao halali vya chama.

CAG afanye ukaguzi

Mara baada ya uamuzi huo, Maalim Seif alizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wabunge wa CUF Magomeni, Dar es Salaam na kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufanya ukaguzi wa fedha za ruzuku za chama hicho.

Alisema baada ya uamuzi huo wa Mahakama ni vyema CAG, akafanya ukaguzi kwa kuwa bodi hiyo ya Profesa Lipumba haikuwa halali.

“Tumeupokea kwa furaha uamuzi wa Mahakama Kuu, umekata mzizi wa fitina wa madai yetu dhidi ya Rita. Nilishasema toka awali tutapokea uamuzi wowote wa Mahakama utakaotolewa,” alisema.

“Nawaomba wanachama wa CUF wawe watulivu kwa sasa wakati tukisubiri uamuzi mwingine utakaotolewa Ijumaa,” aliongeza Maalim Seif.

Uamuzi wa Ijumaa utakaotolewa mahakamani hapo, utahusu uhalali wa Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti baada ya kutangaza kujiuzulu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Profesa Lipumba alitangaza uamuzi huo kwa kile alichoeleza kutoridhishwa kwake na uamuzi wa vyama vilivyoshirikiana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kumpokea na kumpitisha Edward Lowassa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Profesa Assad kuhusu wito huo wa ukaguzi ndani ya CUF na alisema bado hajapata taarifa rasmi kuhusu ofisi yake kuombwa kufanya ukaguzi maalumu katika chama hicho.

“Ndio kwanza nasikia kwako hizi taarifa za kuombwa nifanye ukaguzi, siwezi kusema lolote kwa sasa. Lakini ikija taarifa official (rasmi), nitaiangalia kwanza,” alisema Profesa Assad.

Kesi ilivyoanza

Jaji Masoud alitoa uamuzi huo kufuatia kesi iliyofunguliwa na mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh anayetoka kambi ya Maalim Seif, anayewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Fatma Karume; dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Saleh ambaye pia ni mwanasheria na mwanahabari kitaaluma alifungua kesi hiyo akipinga uamuzi wa Rita kuwaidhinisha na kuwasajili wajumbe waliopendekezwa na kambi ya Profesa Lipumba na kuweka kapuni majina yaliyopendekezwa na kambi ya Maalim Seif.

Mbunge huyo alikuwa akidai kuwa wajumbe hao waliosajiliwa hawakuwa halali kwa kuwa hawakupatikana kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Wajumbe hao walioidhinishwa na Rita ambao pia walikuwa wadaiwa katika kesi hiyo ni Peter Malebo, Hajira Silia, Azizi Dangesh, Amina Mshamu, Abdul Magomba, Asha Suleimani, Salha Mohamed, Suleiman Issa na Musa Kombo.

Uamuzi huo umekuja siku nne kabla ya Ijumaa hii kutolewa uamuzi mwingine kuhusiana na uhalali wa Profesa Lipumba kurejea katika nafasi yake hiyo ya uenyekiti baada ya kutangaza kujiuzulu mwaka 2015.

Hata hivyo, licha ya Mahakama kuamua kuwa majina ya pande zote hayakuwa na sifa za kusajiliwa kuwa wajumbe wapya wa bodi hiyo, uamuzi huo umeonekana kuinufaisha kambi ya Maalim Seif kwani mawakili wake, Juma Nassoro na Daim Halfan walionekana kuufurahia.

“Sisi kwetu tulichokuwa tunapinga ni hao waliosajiliwa hawakuwa wajumbe halali. Kwa kuwa wao ndio waliokuwa wamesajiliwa sasa Mahakama imesema kuwa si halali, hicho ndicho tulikuwa tunakitaka,” alisema Wakili Halfan.

Naye wakili Nassoro alisema kwa uamuzi huo, sasa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho wataendelea na majukumu hayo hadi hapo wajumbe wengine watakaposajiliwa kihalali.

Wakati mawakili wa kambi ya Maalim Seif wakionyesha kufurahia uamuzi huo, wakili wa kambi ya Profesa Lipumba, Mashaka Ngole alisema watakachofanya ni kuitisha kikao ili kufanya uteuzi mpya kwa kuzingatia matakwa hayo ya kisheria. “Kwa sasa nimeitwa kwenye kikao, lakini tulishakubaliana kwamba tunaitisha kikao rasmi ili kufanya uteuzi upya,” alisema Wakili Ngole.

Wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif, ambao hawakusajiliwa na Rita na ambao Saleh alikuwa anataka Mahakama itamke kuwa ni wajumbe halali ni Abdallah Khatau, Joran Bashange, Ali Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed na Yohana Mbelwa.

Si Lipumba wala Maalim Seif

Hata hivyo, Jaji Benhaji katika uamuzi wake amesema majina ya pande hizo zote hayakuwa na sifa kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hiyo kwa kuwa walipendekezwa kinyume cha Sheria ya Muungano wa Wadhamini, kwani hapakuwa na kikao halali kilichowapendekeza. “Kwa sababu hizo, kwa maoni yangu ni kwamba kwa kuzingatia kifungu cha 17 cha Sheria ya Muungano wa Wadhamini, hakuna hata mmoja aliyestahili kusajiliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini,” alisema Jaji Masoud na kusisitiza:

“Kama mdaiwa wa kwanza (Rita) angezingatia matakwa ya sheria, hawa wote (majina ya pande zote mbili yaliyokuwa yamependekezwa) hawastahili.”

Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, mambo yanayotakiwa kuzingatiwa na Rita katika kusajili wajumbe wa bodi za taasisi au bodi ni kuwepo kwa mkutano halali wa taasisi au bodi husika ulioteua au kupendekeza majina.

Jambo lingine ni mkutano huo uwe umesimamiwa na mamlaka halali ya kiserikali.

Hata hivyo, alisema katika ushahidi wa mashahidi wote wa pande zote pamoja na vielelezo vyote vilivyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote wakati wa usikilizwaji, hakuna mahali ambapo imeelezwa na shahidi yeyote wala kielelezo chochote kama matakwa hayo yalizingatiwa.

Akizungumzia madai na ushahidi wa mdai (Saleh) alisema kulikuwa na mkanganyiko hasa kuhusiana na muda wa kuisha kwa bodi ya awali na lengo la usajili wa wajumbe wapya.

Alibainisha kuwa Saleh katika hati yake ya madai alidai kuwa muda wa wajumbe wa bodi wa awali unaisha mwaka 2017, lakini wakati akitoa ushahidi wake mahakamani alieleza kuwa muda wa wajumbe wa bodi wa awali unakwisha mwaka 2019.

Pia Jaji Masoud alisema kuwa Saleh katika ushahidi wake alieleza kwamba majina yaliyopendekezwa yalikuwa ni kwa ajili ya kujazia nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi tu, huku akisema kwamba mkanganyiko huo hauwezi kufumbiwa macho.

Imeandikwa na James Magai, Bakari Kiango (Dar) na Muhammed Khamis (Zanzibar)



Chanzo: mwananchi.co.tz