Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mbunge Chadema ahoji mkataba wa Barrick, Serikali ya Tanzania

93649 Pic+heche VIDEO: Mbunge Chadema ahoji mkataba wa Barrick, Serikali ya Tanzania

Thu, 30 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri kivuli wa Madini nchini Tanzania, John Heche amehoji mambo manne kuhusu mikataba tisa ambayo Serikali ya Tanzania imesaini na kampuni ya Barrick Gold Ijumaa ya Januari 24, 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 29, 2020 mjini Dodoma, Heche ambaye ni mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), amesema katika makubaliano hayo mambo mengi yamefichwa.

Makubaliano kati ya Serikali na Barrick yaliyoshuhudiwa na Rais John Magufuli ni matunda ya mazungumzo kati ya Serikali na kampuni hiyo tangu mwaka 2017 yaliyozaa kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu ulianza mwaka 2017 na Magufuli akaunda tume kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili.

Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick, mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga ikachukua nafasi yake.

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Heche amesema Chadema watailazimisha Serikali kupeleka mikataba yote tisa ili ukweli ujulikane.

“Faida za kiuchumi katika mkataba huu  ni zipi na kwa nini haziwekwi wazi. Uwazi  kuhusu asilimia 16 za hisa za Tanzania ni upi. Ziko wapi Sh426 trilioni walizokuwa wanadaiwa hao Barrick na kwa nini wameruhusu Serikali kushtakiwa nje wakati walishakataa.”

Heche amesema katika taarifa ya uchunguzi wa kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma walibaini kulikuwa na madini mengi katika makontena ya makinikia yaliyokuwa na thamani kubwa lakini yote yamefichwa.

Heche amesema fedha walizokuwa wakidaiwa kampuni hiyo walipaswa kuzilipa kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema sheria hiyo inaeleza kuwa kodi ikishakadiriwa hakuna namna ya kubatilisha hadi  Waziri atangaze katika gazeti la Serikali (GN).

Alitaja sheria ya madini ya mwaka 2017 katika vifungu vya 4, 9, 11 na 12 kuwa vinakinzana na  mkataba ulioingiwa na Serikali.

Amesema sheria hiyo ambayo ilipitishwa kwa hati ya dharura pamoja na mambo mengine ilizuia makinikia kusafirishwa nje ya nchi na pia kesi kusikilizwa nje ya nchi, kwamba kwa muundo ulivyo yote yameachwa jambo alilodai Serikali itakuja kufilisiwa kama kutatokea shida.

Mikataba iliyosainiwa

Mikataba iliyosainiwa ni mkataba wa msingi wa makubaliano, menejimenti na utoaji huduma, mkataba wa wanahisa wa kampuni ya Twiga, mkataba wa wanahisa wa North Mara.

Mingine ni mkataba wa wanahisa wa Bulyankuru, mkataba wa wanahisa wa Buzwagi, mkataba wa maendeleo ya mgodi wa North Mara, mkataba wa maendeleo ya mgodi wa Bulyanhulu na mkataba wa maendeleo wa mgodi wa Pangea.

Chanzo: mwananchi.co.tz