Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mambo yanayomsubiri Bernard Membe

Video Archive
Mon, 2 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni upi utakuwa mwelekeo mpya na hatima ya kisiasa ya aliyekuwa kada wa CCM, Bernard Membe baada ya kufukuzwa katika chama chake? Hili ndilo swali kubwa ambalo wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanahitaji majibu yake, ambayo yatatoka kwa Membe mwenyewe.

Membe baada ya kufukuzwa CCM juzi aliliambia Mwananchi kwamba kufukuzwa kwake kumetokana na uamuzi wake wa kutaka kugombea urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu na kwamba anafurahi kwamba sasa yuko huru.

“Nafurahi sasa niko huru, nitafanya mambo yangu kwa uhuru bila kuhojiwa na kuulizwa ulizwa na mtu yeyote. Si unajua nimefungua kesi mahakamani na hii ni kesi ya kisiasa,” alisema na kuongeza:

“Kuwepo wangu CCM kulikua kunanifunga kutozungumza baadhi ya mambo, lakini sasa, kwanza nitakuwa na muda mzuri wa kuifuatilia na pili hakuna mtu atakayenipangia nini cha kufanya katika kesi ile.”

Membe alikuwa akirejea kesi aliyomfungulia Cyprian Musiba katika Mahakama Kuu kwa madai kwamba alimkashifu.

Membe alipewa adhabu ya kufukuzwa yakiwa ni matokeo ya tuhuma za utovu wa nidhamu zilizokuwa mbele ya Kamati Kuu ya CCM, akishtakiwa pamoja na wenzake wawili ambao ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Wakati Makamba akisamehewa, Kinana alipewa adhabu ya karipio ambayo inamweka chini ya uangalizi wa miezi 18 na katika kipindi hicho hataruhusiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya CCM lakini anaruhusiwa kupiga kura.

Vigogo hao waliingia matatani baada ya sauti zao na za wanachama wengine watatu kusambaa katika mitandao ya kijamii, wakizungumzia kuporomoka kwa CCM chini ya Rais John Magufuli, hali iliyoibua mjadala mkali ndani na nje ya chama hicho tawala.

Wanachama wengine walioingia matatani pamoja na vigogo hao ni wabunge; January Makamba (Bumbuli), Nape Nnauye (Mtama) na William Ngeleja (Sengerema) ambao walisamehewa baada ya kumwomba radhi, Rais Magufuli na msamaha huo kuridhiwa na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Mwanza, Desemba 13 mwaka jana.

Uchambuzi wa kisiasa

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania wanasema kwa kuwa safari ya kisiasa ya Membe ndani ya CCM imeingia doa, sasa atapaswa kuchukua hatua muhimu iwapo bado anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais.

Juzi mara baada ya CCM kutangaza kumfukuza uanachama, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa alisema “ndoto haifi” kama alivyowahi kusema Rais wa kwanza mzalengo wa Afrika Kusini, “muda utasema na watu watazungumza”.

Evarist Chahali ambaye alipata kuwa mmoja wa makachero katika Idara ya Usalama wa Taifa ambaye sasa anaishi nchini Uingereza katika uchambuzi wake anasema:

Membe anaweza kufanya moja kati ya mambo matano ambayo ni kukubali matokeo na kuamua kuachana na siasa au kukataa matokeo lakini akakutana na vikwazo kupitia vyombo vya serikali na dhana ya tatu ni kukubali matokeo na kuamua kujiunga na chama cha upinzani.

Chahali anaongeza kuwa Membe anaweza kukataa matokeo na kuamua kutafuta haki yake ndani ya CCM na dhana ya tano ni mwanasiasa huyo kukataa matokeo na kuamua haki yake nje ya kilichokuwa chama chake.

Nje ya dhana za Chahali, pia zipo dhana nyingine, mojawapo ikiwa ni iwapo Membe ataamua kuanzisha chama cha siasa au ataamua kuvumilia na baadaye kuomba radhi kama ilivyowahi kutokea kwa wanachama wenzake wa CCM.

Wanachama hao ambao walifukuzwa lakini baadaye wakarejeshewa uanachama baada ya kuomba radhi ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), Sophia Simba na Salum Madenge ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kinondoni.

Wengine wenyeviti wa CCM wa mikoa minne, Erasto Kwirasa (Shinyanga), Christopher Sanya (Mara), Jesca Msambatavangu (Iringa) na Ramadhani Madabida (Dar es Salaam).

Mwelekeo wa Membe

Kauli za Membe mara baada ya kufukuzwa CCM hazionyeshi mwanasiasa huyo kuwa na mwelekeo wa kuitelekeza siasa, bali ni dhahiri ataendelea kuwa mwanasiasa na hapo swali linabaki katika uelekeo upi?

Dk Muhidin Shangwe wa kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala Bora cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema Membe anaweza kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi dhidi yake au kuhamia upinzani kwa kuwa sheria zilizopo ili uwe rais lazima utokane na chama cha siasa.

“Kustaafu siasa haonekani kama inawezekana na sioni hiyo subira, njia ni kupinga uamuzi mahakamani lakini ukifuatilia matamshi yake, kuna viashiria kama atahamia upinzani,” alisema Dk Shangwe.

Mhadhiri huyo aliongeza, “hali ya kisiasa na anavyojitanabahisha na kama ana ndoto ya urais na ukifuatilia matamshi na tabia zake, anaweza kuhamia upinzani na kauli za wanasiasa wa upinzani kama wanamwalika. Kuna hizo ishara.”

Dhana hiyo ya Dk Shangwe inaungwa mkono na uchambuzi wa Chahali anayesema huu si mwisho wa Membe kisiasa na akimtaja mwanasiasa huyo kuwa ni “high value target” (mlengwa mwenye thamani kubwa) kwa wapinzani.

“Kwa kuzingatia kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, anaweza kupewa fursa ya ‘kulipa kisasi’ dhidi ya Magufuli kwa kupitishwa kuwa mgombea wa chama cha upinzani,” anasema Chahali.

Chahali anasema ikiwa dhana hiyo itafanikiwa basi Membe anaweza kuwa mpinzani wa Magufuli kwenye uchaguzi na kumpa nafasi ya kufanya jaribio jingine la kuwania urais wa Tanzania.

Aliyewahi kuwa kaimu mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima alisema kwa mazingira ya sasa Membe hawezi kuanzisha chama cha siasa kwani mlolongo ni mrefu na inaweza kufika Juni hajamaliza kukisajili.

“Kwa hali ilivyo hili suala la yeye kuingia chama kingine ni sawa, lakini kuanzisha chama wakati huohuo ni mwaka wa uchaguzi itakuwa ngumu. Nafikiri katika hali tuliyonayo ajiunge na chama kingine,” alisema Taslima ambaye sasa ni kada wa ACT—Wazalendo.

Membe aliyezaliwa Novemba 9, 1953, Rondo, Chiponda mkoani Lindi, alikuwa miongoni mwa makada 42 wa CCM waliochukua fomu ya kuwania urais ndani ya chama hicho 2015.

Chanzo: mwananchi.co.tz