Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Chadema yaja na mwelekeo mpya

Video Archive
Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua sera mpya ya mwaka 2018 ambayo imejikita katika masuala ya utawala bora, uchumi wa soko jamii utakaoshirikisha sekta binafsi na kuhakikisha Serikali inatoa huduma bora za jamii.

Kupitia sera hizo ilizoanza kuzitunga kwa mara ya kwanza mwaka 1993 na kuzifanyia mapitio 2006, chama hicho kinaonyesha jinsi gani kitakavyoongoza nchi pindi kikishika madaraka na mahali gani kinakusudia kuwapeleka wananchi na nchi kwa kipindi kirefu kijacho.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam mbele ya wawakilishi wa mabalozi, taasisi za Serikali na viongozi wa dini, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema baada ya hatua hiyo, wataanza kupokea maoni kuhusu sera hizo kutoka kwa wananchi kabla ya kupitishwa na mkutano mkuu wa chama hicho.

“Lengo ni kuwapa wananchi sera yao, kuanzia sasa hii sera ni ya wananchi wote ili utakapofika wakati wa uchaguzi wawe wanajua wanachagua chama cha namna gani na kitawaongoza kuelekea wapi,” alisema Mbowe.

Alifafanua kuwa katika eneo la utawala bora, wanaamini katika uwazi na uwajibikaji serikalini na wananchi kushirikishwa katika kuamua masuala muhimu yanayohusu maisha yao.

Alisema Chadema itawashirikisha wananchi kutoa maoni na mapendekezo katika mchakato wa kutunga sheria zote za nchi ili kurahisisha usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo.

“Chadema itahakikisha inakuza demokrasia kwa kuanzishwa taasisi huru za uchaguzi ili kupata viongozi bora waliochaguliwa kidemokrasia,” alisema Mbowe.

Alisema wananchi watakuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao katika ngazi mbalimbali kupitia michakato kwa mujibu wa sheria na taratibu zitakazowekwa.

Alisema pia kutakuwa na ugatuaji wa madaraka, mapambano dhidi ya rushwa, utawala wa sheria na utoaji haki.

“Tumeweka madaraka makubwa kwa Rais, tumeweka madaraka makubwa kwa Baraza la Mawaziri, katika mataifa mengine wanachofanya ni kugatua madaraka, siyo kukusanya madaraka kwa mtu mmoja,” alisema Mbowe.

Alitolea mfano Kenya ambao wamefanya ugatuzi wa madaraka na wananchi wanachaguliwa kuliko uteuzi kufanywa na Rais pekee.

“Hapa kila uteuzi unamtegemea Rais, hata angekuwa malaika atashindwa,” alisema.

Aliweka bayana kwamba Chadema itahakikisha kwamba nchi inapata Katiba Mpya itakayotokana na mapendekezo ya wananchi na kubainisha kuwa kuhusu Muungano wanataka Serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Katika Sera hiyo, Chadema imesema itazuia kwa nguvu zote utawala usiozingatia sheria, ukamataji holela na ubambikaji kesi kwa wananchi wasio na hatia.

Kuhusu rushwa, sera hiyo inasema Chadema itaanzisha taasisi huru ya kuzuia na kupambana na rushwa, itaimarisha uwezo wa Bunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali na kuweka mgawanyo mzuri wa dola yaani Bunge, Serikali na Mahakama.

Mbowe pia alisema chama hicho pia kitaimarisha Serikali za majimbo, kikiwa kimeunda majimbo 10; manane Tanzania Bara na mawili Zanzibar pamoja na kuweka mfumo wa uongozi wa majimbo kuwa wa kuchaguliwa.

Alisema kwa sasa nafasi nyingi za uongozi ni uteuzi wa Rais na kila uamuzi unategemea mtu mmoja na eneo moja, jambo ambalo alisema wanataka libadilike ili madaraka yarudi kwa wananchi kupitia majimbo.

Kuhusu umiliki wa ardhi, sera hiyo inaweka mfumo ambao wananchi watakuwa wanamiliki ardhi pamoja na rasilimali zake, za juu na chini ya ardhi ili kuepuka utaratibu wa sasa ambao unaruhusu Serikali kuchukua ardhi ya wananchi pale inapobaini madini au rasilimali nyingine.

Katika uchumi, Mbowe alisema Chadema itajikita kulenga uchumi wa soko unaozingatia maendeleo na ustawi wa jamii kwa kushirikisha sekta binafsi.

“Msingi wa mfumo huu wa uchumi ni kujenga na kuruhusu ushindani, soko huria na sekta binafsi kumiliki mali,” alisema Mbowe.

Aliutaja mkakati jumuishi wa uchumi wa taifa kuwa ni kuimarisha uchumi kukabiliana na changamoto za ajira, bei ya bidhaa, mfumo wa kodi unaotabirika, uwiano kati ya mauzo nje ya nchi, kuagiza kutoka nje na kusimamia Deni la Taifa ili kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuondokana na umaskini.

“Lengo ni kupinga dhana kuwa umaskini ni sifa, kama ambavyo wengi wanadhani. Umaskini siyo sifa, ni laana. Sisi tunataka watu wote wawe matajiri,” alisema Mbowe.

Alifafanua kuwa wanaamini mafanikio ya mtu mmojammoja ndiyo mafanikio ya taifa, hivyo watakuwa ni viongozi wenye kuuchukia umaskini na kujadili namna ya kupambana nao badala ya kuhubiri jinsi ya kuwaongoza watu maskini.

Alitumia muda mrefu kueleza nchi ilikopita tangu uhuru, huku akisema mambo mengi yaliyofanyika siku zilizopita, ikiwamo sera ya ujamaa, yamesababisha wananchi wamekuwa na umaskini wa fikra.

“Bora kuwa maskini wa mali kuliko kuwa maskini wa fikra, hili ni jambo baya,” alisema.

Mbowe alisema baada ya kuhakikisha sekta binafsi inahusika kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi, Serikali itaachiwa fursa ya kutoa huduma za jamii kwa wananchi kwa kuwa ndilo jukumu lake.

“Kumejengeka dhana kuwa huduma za kijamii kama hospitali, shule, zahanati zimejengwa na Serikali ni kama msaada au ofa. Kiuhalisia, haya yote ni jukumu la Serikali,” alisema Mbowe.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa alisema kwa mara ya kwanza, Watanzania watapata sera ya chama ambayo wanapaswa kuipitia na kuitolea maoni kabla haijapitishwa na mkutano mkuu.

Alisema, “Waichambue, waipitie, waitolee maoni ambayo yatachukuliwa na kufanyiwa kazi.”

Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye alisema maoni kuhusu sera hiyo yanapokewa katika ofisi za chama hicho katika maeneo yote ambako viongozi wake wanapatikana.

Alisema anajua kuna watu watakaoibeba na kuipinduapindua, lakini wataipapasa na hawatafanya kinachokusudiwa.

Sumaye alisema sera hiyo ni ya wananchi na Chadema na wamefanya kama ambavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ni lazima chama cha siasa kiwaeleze wananchi namna kitakavyowaongoza.

Alisema ana hakika kwa sera hizo na kukiwa na uchaguzi huru, Chadema itachukua nchi na kuiongoza kama ilivyoainisha.

Akimkaribisha mwenyekiti kuzindua sera hizo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema sera hiyo inalenga kujenga taswira ya chama kwa wananchi ili kuzungumza lugha moja katika kujenga uchumi na umoja wa kitaifa.

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alisema uzinduzi huo unatoa fursa kwa wananchi kuichambua, kuinyumbulisha na kuiona.

Alisema unapofika uchaguzi watakuwa wanawashindanisha wagombea wao dhidi ya sera za vyama vyao kwa uwazi.

Soma Zaidi: Chadema yazindua sera mpya

Chanzo: mwananchi.co.tz